SALUM Abubakar ‘Sure Boy’ amepewa ruhusa ya kujiunga na Yanga ama klabu yoyote inayomuhitaji kama wataenda mezani na kuafikiana kuhusu dau.
Sure Boy amecheza kwa mafanikio makubwa katika kikosi cha Azam FC kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10 sasa huku kukiwa na taarifa ya Yanga kuhitaji huduma yake.
Zakaria Thabith ‘Zaka Zakazi’, Ofisa Habari wa Azam FC amesema wao wako tayari kumuuza mchezaji huyo, hivyo wanamkaribisha yeyote anayemtaka.
“Tunasikia kuwa kuna baadhi ya timu zinamuhitaji mchezaji wetu Salum, sisi tunachojua ni kuwa bado mchezaji huyo ana mkataba na Azam lakini hilo haliondoi uwezekano wa kumpata kwa klabu yoyote inayomuhitaji.
“Unajua kuna wakati wachezaji wanaweza kuvutiwa na mkakati fulani kutoka klabu nyingine jambo ambalo linakubalika, hivyo kama Yanga watakuja mezani tukazungumza na mchezaji mwenyewe akaridhia basi sisi hatuna kipingamizi tutaruhusu aende,” amesema Zaka Zakazi.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema: “Kwa sasa niwatoe hofu mashabiki na wapenzi wa Yanga kuwa mambo mazuri yanakuja ila waendelee kuwa na subira kila kitu kitakuwa wazi.
Chanzo: Championi
Post a Comment