MWEKEZAJI wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ ameonekana kupania kuwabakisha mastaa wake wote muhimu wanaomaliza mikataba yao, na sasa ni zamu ya kiungo mkabaji Mzamiru Yassin na beki Muivory Coast Pascal Wawa ambao wapo kwenye mazungumzo ya mwisho kukamilisha usajili wao.
Mzamiru ni kati ya wachezaji watano ambao mikataba yao inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu, wengine ni Wawa, Shiza Kichuya, Sharraf Eldin Shiboub, Yusuph Mlipili na Dilunga.
Taarifa zinaeleza kuwa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba inayoongozwa na Mo iliketi kuzungumza kwa ajili ya kuhakikisha anaongeza mkataba mpya wa kukipiga Msimbazi.
Aliongeza kuwa tayari mazungumzo yanakwenda vizuri na huenda kiungo huyo akasaini mkataba wa miaka miwili ya kuichezea Simba kama ilivyokuwa kwa Dilunga ambaye muda wowote ataongeza mkataba wa kuichezea timu hiyo.
“Kwa mujibu wa ripoti ambayo kocha Sven (Vandenbroeck) aliitoa kwa viongozi, Mzamiru ataendelea kuwepo kwenye usajili wa msimu ujao, hivyo tayari viongozi wapo kwenye hatua za mwisho kukamilisha mipango hiyo ya kumbakisha.
“Wapo wachezaji wengine ambao tayari viongozi wameanza mazungumzo nao ambao mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu huu na hiyo yote ni katika kuepukana na presha mwishoni mwa msimu kutoka kwa timu pinzani watakaowahitaji wachezaji hao.
“Baada ya Dilunga dili lake kukamilika hivi sasa viongozi wamegeukia kwa Mzamiru ambaye yeye mwenyewe ameonyesha nia ya kubakia Simba, kama mambo yakienda sawa atapewa mkataba kwa ajili ya kuupitia,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Mzamiru kuzungumzia hilo alisema: “Ni kweli tumeanza mazungumzo ya awali na timu yangu ya Simba, kama tukifikia muafaka mzuri basi nitaongeza mkataba.”
Chanzo: Championi
Post a Comment