Na Saleh Ally
TUMEKUWA tukijadili sana kuhusiana na soka la Mkoa wa Tanga na bila shaka, Coastal Union na watani wao African Sports ndio wanapaswa kuwa msitari wa mbele katika maendeleo yake.


Katika historia ya soka nchini, timu hizi mbili kwa ujumla ni kubwa na zinazungumzwa kutokana na kuwa na rekodi za kubeba ubingwa wa Bara na ule wa Muungano. Hakuna ubishi, ni klabu kongwe na kubwa.


Unapozungumzia mchezo wa soka Mkoa wa Tanga ambako kuna wapenda soka wengi sana, lazima utazitaja klabu hizi kubwa na kongwe.


Bila ya ubishi ukongwe na ukubwa wa majina wa klabu hizi mbili, umekuwa haufanani hata nusu ya robo ya mandeleo ambayo zimefikia. Zaidi ni maneno mengi, lawama, majungu na chuki.


Tunakubaliana katika mpira wa Tanzania, suala la chuki limepewa nafasi kubwa na linaweza hata kushindana na ukweli na uhalisia. Lakini mara nyingi tusingependa kukubali ukweli.




Mnakumbuka kila namna ambavyo nimeisema Coastal kuhusiana na hili na watu wengi wapenda mpira kutoka Tanga wakalaumu. Huenda wanaamini kuambiwa ukweli ni kusakamwa au kutopendwa. Si vibaya maana kila mwanadamu angependa masikio yake yalishwe maneno matamu, maneno ya furaha. Lakini vizuri kupokea yale yanayokera masikio yako yanayoweza kukusaidia kubadilika.


 Muda mwingi Coastal Union hawakuwa makini, mwendo wao haukuendana na jina na ukongwe wao lakini tuwe wakweli, mnyonge mnyongeni haki yake mumpe na safari hii pamoja na juhudi nyingine, Kocha Juma Mgunda anastahili kupewa haki ya kufanya vema.


Mgunda kajitahidi sana, mwendo wanaokwenda nao Coastal Union tunauona, usiwaze sana kuhusiana na pointi walizozikusanya tu lakini angalia ya uchezaji wa kikosi chao katika kila mechi, utaona ni timu iliyofundishwa na hasa inafuata mifumo sahihi ya mafunzo.


Kila timu iliyocheza dhidi ya Coastal Union bila ya kujali imeshinda au kufungwa, itakueleza ugumu wa timu hiyo ya Tanga na ubora wa soka lake na hii ni sehemu ya kazi nzuri ya Kocha Mgunda.


Tunajua Mgunda ni gwiji wa Coastal Union, wachezaji waliofanya vizuri wakati wa Coastal iliyo imara na mfano, leo kama kocha amebadilisha mambo, bila ya wachezaji maarufu sana au rundo la wachezaji wa kigeni, wengi ni vijana tu lakini kazi ni nzuri na inaonekana haswa.

  
Baada ya mechi 24 za Ligi Kuu Bara, Coastal wako katika nafasi ya tano, wakiwa wamekusanya pointi 39 ambazo zinazidiwa na Yanga, Namungo, Azam FC na vinara Simba.


 Bila ya ubishi unaona, kama utazungumzia ulinzi, basi safu ya ulinzi ya Coastal ni kati ya zile zilizo bora, kwani katika mechi hizo 24, wameruhusu mabao 12 ukifananisha na timu kama Singida imeruhusu mara 36, Mbao FC mara 31, KMC mara 30, au Alliance, Mbeya City na Mwadui kila moja mara 29.


 Ukiangalia upande wa safu za ushambulizi, pamoja na kuwa na chipukizi wengi katika safu yake hiyo, kikosi cha Mgunda kimefunga mabao 24 ambayo ni mengi zaidi ya timu nyingine takriban 13 zinazoshiriki ligi hiyo.


Hauwezi ukasema Mgunda ndiye kocha bora zaidi kwa sasa katika Ligi Kuu Bara lakini kama utatoa timu za Dar es Salaam, kwa zile za mikoani, yeye ndiye kocha bora zaidi mzalendo kwa kipindi hiki.


 Ubora huu wa Mgunda na namna alivyowatuliza mashabiki wa Coastal Union ambao wamekuwa na kiu cha ushindi muda mwingi, inaonyesha kuna watu huenda huwa tunawachukulia poa kwa kuwadharau lakini uwezo wao ni mkubwa sana.


Mgunda ana uwezo mkubwa na itakuwa vizuri Wanatanga kumshika mkono na kutembea naye vizuri kwa kuwa inaonekana kuna mambo ambayo yaliwashinda anaweza kubadilisha na itakuwa kheri kwenu kwa kuwa ni mtu wa hapo nyumbani Tanga.


Mgunda ameonyesha asingependa kushauriwa, tena amesema kwa vitendo na hili vema likapewa kipaumbele kwa kuwa akitumika vizuri ataanza kuisaidia Tanga lakini baadaye, ataisaidia Tanzania kwa ujumla.


Binafsi nimpongeze na kumpa moyo Kocha Mgunda, nimkumbushe kutobweteka na badala yake aifanye vizuri kazi yake kwa weledi na siku moja awe kocha bora zaidi Tanzania kuzidi wageni

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.