STAA wa Simba, Mnyarwanda, Meddie Kagere, amesema kuwa kitu kilichompa ukame wa mabao katika michezo minne ya Ligi Kuu Bara ni kupaniwa na mabeki wa timu pinzani na siyo kitu kingine.

 

Hayo aliyasema ikiwa ni baada ya kufunga bao lake la 14 katika msimu huu wa ligi wakati timu hiyo ilipocheza na Biashara United kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku timu hiyo ikifanikiwa kupata ushindi wa mabao 3-1.

 

Michezo hiyo minne ambayo Kagere alitoka patupu bila ya kufunga mabao huku akiwa uwanjani ni dhidi ya Lipuli FC, Mtibwa Sugar, JKT Tanzania na Polisi Tanzania.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Kagere alisema kwake anajisikia furaha kuona akikabwa huku wakiwaachia wachezaji wenzake John Bocco, Hassani Dilunga, Francis Kahata na wengine wakifunga mabao.

 

Kagere alisema hivi sasa anafurahia uwepo wa Bocco katika kikosi cha kwanza, wakicheza pamoja kunawavuruga mabeki na kushindwa kumjua mshambuliaji yupi wamzuie asifunge mabao tofauti na ilivyokuwa awali wakati kocha wa timu hiyo, Mbelgiji Sven Vandenbroeck akitumia mshambuliaji mmoja na kiungo katika safu hiyo.

 

Aliongeza kuwa mashabiki wa Simba wajiandae kumuona akiendelea na kasi yake ya kufunga mabao katika michezo ijayo baada ya kocha kubadili mfumo wa kuwatumia washambuliaji wawili.

 

“Lipo wazi katika kila mchezo mabeki wananiangalia mimi pekee kabla ya kocha kubadili mfumo akitutumia washambuliaji wawili badala ya mmoja, awali hicho ndicho kilichokuwa kinanipa ugumu wa kufunga.

 

“Lakini nafurahi wakati mabeki hao wa timu pinzani wakiniangalia mimi, wachezaji wengine wanafunga na kufanikiwa kupata matokeo mazuri ya ushindi ambacho ndiyo kitu cha umuhimu kwangu.

 

“Mashabiki wajiandae kupata furaha katika michezo mingine inayofuata ya ligi wakiniona nikiendelea na kasi yangu kama ilivyokuwa mwanzoni mwa ligi,” alisema Kagere

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.