Akizungumza na Mwanaspoti, Salamba alikiri kwa sasa hayupo nchini huku akificha kueleza mahali alipo japo Mwanaspoti linafahamu.
NJIA ndio imeanza kufunguka kwa straika wa Simba, Adam Salamba ambaye amepelekwa kukipiga kwa mkopo kule Namungo ya Ruangwa mkoani Lindi.
Straika huyo mwenye utulivu anapokuwa jirani na goli la upinzani, kwa sasa yuko nchini Kuwait akikamilisha dili lake la kukipiga klabu ya Al-Jahra SC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini humo.
Kama mambo yatakwenda kama yalivyopangwa basi Salamba atasaini mkataba wa miaka mitano na matajiri hao wa mafuta na gesi, ambao wameweka ofa ya mamilioni ya shilingi ambazo Simba watavuna kama ada ya uhamisho.
Mbali na Simba, hata Salamba mwenyewe amewekewa dau tamu la usajili kwenye ofa hiyo na sasa anakamilisha mazungumzo ya mwisho kabla ya kumwaga wino.
Mwanaspoti ambalo lina nakala ya ofa ambayo Al-Jahra SC wamempa Salamba na mabosi wa Simba, ikiwa tayari kulipa Dola za Marekani 45,000 (Zaidi ya Sh100 milioni) ambazo zinaweza kuwa kwa ajili ya Simba yenye mkataba naye.
Pia, matajiri hao wametenga Dola 5,000 (Tsh11,487,000) kwa ajili ya Salamba mwenyewe pamoja na kumtengea mshahara wa Dola 4,000 (Tsh9,189,590) kwa mwezi. Ofa nyingine ni nyongeza ya mshahara kwa asilimia 25% ambayo itategemea kiwango chake uwanjani.
Mbali na yote hayo, matajiri hao wamemwandalia Salamba ndinga ya maana pamoja na makazi yenye fenicha za kibabe ndani huku pia ikimwandalia tiketi ya ndege kila anapotaka kurejea nchini kwa mapumziko.
SALAMBA AFUNGUKA
Akizungumza na Mwanaspoti, Salamba alikiri kwa sasa hayupo nchini huku akificha kueleza mahali alipo japo Mwanaspoti linafahamu.
“Ni kweli kwa sasa sipo Tanzania, nimeondoka kwa ajili ya kukamilisha mazungumzo na moja ya klabu ambayo inahitaji huduma yangu. Kama mambo yatakwenda sawa basi nitakuwepo huku kutimiza ndoto zangu za kucheza soka la kulipwa nje ya nchi,” alisema Salamba.
Ofa hiyo imekuja ikiwa ni mwezi tu tangu Salamba ajiunge na klabu ya Namungo FC kwa mkopo akitokea Afrika Kusini alipokwenda kufanya mazungumzo na klabu ya TS Sporting.
Hata hivyo, mazungumzo hayo hayakwenda vizuri na kuamua kurejea zake nyumbani.
Salamba alijiunga na Simba kwa dau la Sh30 milioni pamoja na ndinga aina ya Toyota Crown, akisaini mkataba wa miaka miwili. Kabla ya kutua Simba, Salamba alikuwa akiwindwa na Yanga wakati huo akikipiga Lipuli FC akitokea Stand United, lakini wababe hao wa Jangwani walipigwa bao kutokana na kutokuwa vizuri kiuchumi.
Bao lake la kwanza akiwa Simba SC lilikuwa dhidi ya Mouloudia Club of Oujda Uwanja wa Kartepe Green Park mjini Istanbul wakati walipoweka nchini Uturuki.
Hata hivyo, kwenye TPL bao lake la kwanza lilikuwa dhidi ya Alliance kwenye ushindi wa mabao 5-1 Uwanja wa Taifa, Novemba 14 mwaka jana.
VIONGOZI FRESHI TU
Katibu wa Namungo FC, Ally Seleman alisema tayari wamemruhusu Salamba kuondoka baada ya kupata timu nje ya nchi, hivyo hawana sababu ya kumng’ang’ania.
“Tulimchukua kwa mkopo kutoka Simba, ambao walituomba tumwachie na hilo halikuleta shida japo alikuwa katika mipango ya benchi la ufundi kwa msimu huu wa ligi,” alisema Seleman.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi alipoulizwa juu ya hilo alisema: “Sina taarifa hizo labda aulizwe Magori (Crescentius Magori, Mtendaji Mkuu wa klabu).”
Mwanaspoti lilimsaka, Magori kwa njia ya simu bila mafanikio yotote kwani, simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa.
HII NDIO AL JAHRA SC
Ilianzishwa mwaka 1966 ikijulikana kama Al-Shuhada, lakini mwaka 1972 ikabailishwa jina na kiitwa Al-jahra SC na jina la utani ikifahamika kama ‘Sons of the Martyrs’. Msimu wa mwaka 2017/18 ilimaliza nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Msimu uliopita timu hiyo ilishuka daraja baada ya kumaliza nafasi ya tisa katika ligi yenye timu 10 ikimaliza msimu ikiwa na alama 15 ikishinda mechi nne na sare tatu na sasa itaonekana Ligi Daraja la Kwanza ‘Kuwaiti Division One’
Timu hiyo inanolewa na Boris Bunjak, ambaye mwaka 2012 aliifundisha Azam FC kabla ya kutimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Stewart Hall.
Post a Comment