ILIPOISHIA juzi Jumanne katika makala haya yanayomhusu mwanachama na mmoja wa viongozi wa Yanga, aliyeibukia kutoka kuwa dereva hadi meneja.
Juzi tuliwaletea mambo mbalimbali yanayofanya atembee kifua mbele kulitumikia chama hilo, ambapo pamoja na mambo mengine alieleza alivyoishia kulazwa baada ya kichapo walichokipata kutoka Simba na alivyojiweka rehani ili timu iachiwe ikakipige katika michuano mbalimbali..SASA ENDELEA
YANGA ILIMFILISI
Wakati kuna mashabiki wanatoa maneno makali kwamba wanaumizwa na matokeo mabaya ya Yanga na kuwatukana wachezaji, makocha na viongozi kitu ambacho hakina msaada kwa timu, kwa Hafidh Saleh ni tofauti kwani yeye yupo tayari kutumikia kiasi chake cha pesa kwa ajili ya timu ili tu iweze kuwa na mazingira mazuri.
Hafidhi anasema hakumbuki ulikuwa ni mwaka gani lakini timu ilikuwa chini ya Kocha Raoul Shungu ambaye alipambana kuhakikisha anakaa sehemu nzuri yeye pamoja na baadhi ya wachezaji kwa kuwapangia nyumba nzima ya kuishi.
“Shungu na wachezaji Method Mogella, Willy Martin, Sekilojo Chambua, Zakaria Kinanda na nyota wengine sikumbuki majina yao niliwapangia nyumba nzima yenye thamani ya laki tisa ambayo miaka hiyo ningeweza kununua hata viwanja vitatu lakini sikufanya hivyo na kuamua kuwapangia wachezaji kutokana na mapenzi niliyokuwa nayo kwa Yanga,” anasema.
“Kuhusu kufilisika kwa ajili ya klabu hiyo, siwezi kusema hivyo kwani nilikuwa nafanya kwa mapenzi na nilikuwa nafurahia kuona timu inakuwa katika mazingira mazuri, nilikuwa sipendi timu ipitie katika shida nilichokuwa nakipata katika biashara yangu nilikuwa tayari kukiwekeza Yanga,” anasema.
“Wengi wanasema kuhusiana na maisha yangu kuyumba kuwa Yanga imechangia, inaweza ikawa sababu lakini sidhani kama hilo lina ukweli, kwani wapo wengi wanaotumia fedha zao kwa ajili ya Yanga. Hii timu imenisomeshea wanangu, hivyo sioni shida nikiwanacho nishindwe kutoa kwaajili ya timu,” anasema.
“Nimefanya kazi chini ya viongozi wanne hadi sasa nilianza na Emmanuel Madega, Llyod Nchunga, Yusuf Manji na sasa Dk. Mshindo Msolla viongozi wote hao nimefanya nao kazi vizuri na kila mmoja alikuwa na mafanikio aliyoiachia klabu,” anasema na kuongeza:
“Manji sitamsahau katika uongozi wake, kwani aliifanyia mambo makubwa klabu alikuwa na mkono wa utoaji, alipambana na ndiye aliyeiingiza timu yetu mara mbili katika makundi tukiwa katika mashindano ya Kombe la Shirikisho,” anasema.
“Yanga kufikia mafanikio hayo ilitokana na usajili aliokuwa anaufanya alikuwa anasajili wachezaji wenye uwezo ambao waliweza kuipa timu mafanikio kwa kutwaa ligi mara tatu mfululizo na kushiriki mashindano ya kimataifa na kufika hatua ya makundi mara mbili,” anasema Hafidh.
“Madega pia aliipa ubingwa Yanga wa ligi na wa Afrika Mashariki hivyo pia namkumbuka kwa uongozi wake bora chini yake nisiwe mchoyo wa fadhila wote ni watendaji wazuri na ndio maana Yanga ipo hadi sasa nikimuelezea mmoja mmoja kwa uzuri sitamaliza leo,” anasema.
“Yanga imefanikiwa kuwasajili nyota wa kimataifa kutoka katika mataifa mbalimbali wengi walifanya mambo makubwa na nimefanya nao kazi vizuri nikiwa kama meneja, nitaendelea kuwakumbuka kwa mazuri na hata mabaya kwani hakuna mwanadamu asiyekosea,” anasema na kuongeza kuwa:
“Miongoni mwa mastaa waliopita Yanga nikiwa meneja miaka ya nyuma ni pamoja na Emmanuel Okwi, Donald Ngoma, Haruna Niyonzima, Yaw Beko, Davies Mwape, Hamis Kiiza na wengine wengi nikianza kutaja hapa sitamaliza Yanga imepitiwa na nyota wengi sana na walikuwa bora,” anasema.
“Soka la Tanzania linakuwa na limekuwa ni ajila kwa vijana wengi wanaojitambua sasa ni muda wa Serikali kuwekeza katika michezo kwa kuandaa bajeti ambayo itadili na michezo tu, ikiwa ni sambamba na kuendeleza michezo mashuleni ambako ndio kuna vipaji vingi vinashindwa kuendelezwa kutokana na kukosa maendeleo ya kusimamiwa.
“Michezo mashuleni imerudi lakini haisimamiwi vizuri ili kuwa bora na kuweza kutoa nyota wengi ambao wanaweza kuwa na chachu kwa timu yetu ya taifa ni kuweka bajeti ambayo inaweza kuwapa morali wachezaji na hata waalimu wanaowafundisha.
“Nikipata nafasi ya kuonana na Waziri wa Utamaduni, Michezo, Sanaa, Dk. Mwakyembe naweza kumwambia arudishe morali mashuleni kuwe na mashindano mbalimbali kama ilivyokuwa miaka ya nyuma lengo ni kuona vipaji vilivyopo mashuleni vinaendelezwa,” anasema.
“Naishi soka napenda sana mpira hata nikiwa nyumbani muda wangu wa mapumziko huwa nafuatilia mpira, mimi ni shabiki mkubwa wa Man United ambayo imekuwa ikizungumzwa sana sikuizi kutokana na matokeo yake, hiyo ndio timu yangu wakati wote,” anasema na kuongeza : “Timu yangu ya Ligi Kuu ya England ni nzuri ningekuwa na uwezo ningembadilisha kocha, ningependa Kocha wa Tottenham, Mauricio Pochettino ndiye angeinoa Man United kutokana na mfumo wake wa ufundishaji kuendana na namna timu yetu inavyocheza kama sio yeye hata Kocha Pep Guardiola anafaa.
“Kukiwa hakuna mechi siku hiyo nitakaa kusikiliza muziki mimi ni Team Kiba mbali na muziki huo napenda ule wa kizamani, nawapenda Msondo Ngoma huwa nasikiliza nyimbo zao, mara baada ya kumaliza burudani, basi nitaanza kufuatilia maendeleo ya wanangu kimasomo,” anasema.
“Kuhusiana na shughuli za nyumbani naomba niwe muwazi sina ninachoweza kukifanya zaidi ya kuchemsha chai na mayai.
“Sijui kupita hiyo kazi huwa namuachia mke wangu, sijawahi kumsaidia kwa lolote ni kutokana na kutofahamu, sina maana mbaya kwamba sio jukumu langu.
“Mke wangu ana busara ananielewa kulingana na mapungufu hayo sio bepari kwamba naamini kupika, kuosha vyombo au kufanya usafi ni kazi ya mwanamke, la hasha sasa usawa ni kwa wote lakini kwangu ni tofauti kutokana na kutoweza majukumu hayo.
“Nimelelewa katika familia yenye watoto wengi wa kike ambao walikuwa wanafanya majukumu hayo kwa usawa wakimsaidia mama, nadhani hiyo inaweza ikawa sababu ya mimi kushindwa kujifunza mambo hayo ya kupikapika na nashindwa kumsaidia mke wangu,” anafunguka Hafidhi ambaye ni mtu mtaratibu sana.
Post a Comment