Mbunge wa Jimbo la Temeke, Abdallah Mtolea, amehojia kanuni za shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kukagua mavazi ya Makocha wa timu za Ligi, huku kukiwa na kundi kubwa la wachezaji ambao hawana bima.
Mbunge Mtolea amehoji suala hilo Bungeni, wakati akiuliza swali kwenda kwa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, juu ya malalamiko ya wachezaji wengi kukosa uhakika wa kupata matibabu kwenye timu zao.
"Wachezaji wengi hawana bima ya Afya, Serikali iko tayari kulishauri Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liachane na kuchunguza makocha wamevaa nini, bali wawatafutie wachezaji bima." amehoji Mtolea.
Akijibu swali hilo Bungeni, Naibu wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Mh. Juliana Shonza amesema watahakikisha wanawashinikiza TFF kulishughulikia suala hilo kwa haraka.
"Kama Wizara tumepokea ushauri, tutaishauri TFF kuhusu bima kwa wachezaji, lakini kuhusu bima za Afya ni jambo la msingi kwa Watanzania wote." amejibu Juliana Shonza.
Mapema jana Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF, lilitoa taarifa kumfungia mechi tatu kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, kwa kukiuka kanuni za mavazi kwenye ligi.
Post a Comment