WACHEZAJI wa kimataifa wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars nahodha Mbwana Samatta, Simon Msuva na Adi Yusuph wanatarajiwa kujiunga na wenzao nchini Burundi kuanzia kesho.
Samatta anayecheza KRC Genk ya Ubelgiji leo atashuka dimbani katika mchezo wa ligi dhidi ya Club Brugge, Msuva yupo na klabu yake ya Difaa El Jajida inayojiandaa na msimu mpya wa ligi ya Morocco na Yusufu jana timu yake ya Blackpool ilitarajiwa kucheza katika ligi ya Championship England.
Taifa Stars inatarajiwa kwenda Bujumbura, wakati wowote kwa ajili ya mchezo wa kufuzu Kombe la dunia 2022 Qatar dhidi ya Burundi utakaochezwa Jumatano. Kocha Msaidizi wa Stars Juma Mgunda alisema wachezaji hao watakutana nao Burundi.
“Wachezaji wengine wote wameshafika isipokuwa hao watakuja moja kwa moja Burundi kuungana na timu, maandalizi yanakwenda vizuri na tuna imani tutafanya vizuri,”alisema.
Alisema mchezo hautakuwa mwepesi wala hawawezi kuwadharau warundi kwasababu ni nchi ndogo, kwani kila mtu anatafuta nafasi ya kusonga mbele. Mgunda alisema vijana wako tayari kupambana na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania.
Baada ya mchezo huo wa kwanza Taifa Stars itarejea Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa marudiano utakaochezwa kwenye uwanja wa taifa Dar es Salaam Septemba 8, mwaka huu.
Post a Comment