NAHODHA na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Burundi, Saido Berahino, amemsifia beki wa Taifa Stars, Kelvin Yondani na kikosi hicho kwa ujumla, baada ya kutinga hatua ya makundi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia, zitakazofanyika Qatar mwaka 2022.
Stars ilitinga hatua hiyo kwa kuichapa Burundi mikwaju ya penalti 3-0, ikiwa ni baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1, matokeo kama ya mechi ya kwanza iliyopigwa Septemba 4, mwaka huu, mjini Bujumbura.
Berahino alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Burundi waliokosa mkwaju wa penalti kati ya watatu waliopiga.
Akizungumza na BINGWA baada ya mchezo huo wa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es salaam, Berahino alisema yeye na wenzake watakuwa wakiendelea kuipa sapoti Stars katika safari yake ya kusaka tiketi ya Kombe la Dunia.
“Taifa Stars ni sehemu ya nchi za Afrika Mashariki, tumefurahi kwa upande wetu, hatukuwa na bahati, tulipata nafasi na kushindwa kuzitumia, hii ni sehemu ya mchezo, mechi ilikuwa nzuri na kila mtu alifurahia,” alisema Berahino.
Berahino alipoulizwa juu ya mchezaji wa Stars aliyemvutia, alijibu: “Wachezaji wote wapo vizuri, ila kwa upande wangu Samatta namkubali zaidi, japo pia yupo yule jezi namba tano (Yondani), alitupa wakati mgumu sana, anajua kukaba, ni beki mzuri sana kwa kweli pamoja na yule mwenzake (Erasto Nyoni).”
Berahino aliyewahi kutamba na Stoke Cityu ya Ligi Kuu England, kwa sasa anakipiga katika klabu ya S.V. Zulte Waregem ya Ubelgiji, akiwa ligi moja na Samatta anayeichezea KRC Genk.
Post a Comment