NA MWANDISHI WETU
EMMANUEL Okwi hayupo tena Simba, John Bocco majeruhi, kukosekana kwao ilitarajiwa Deo Kanda kuvaa vema viatu vyao, lakini bado anaoneakana kuwa na mwendo wa kinyonga na sasa ni zamu ya Ibrahim Ajib.
Hatua hiyo inatokana na aina ya mazoezi yaliyokuwa yakiendelea viwanja vya Gymkana jijini Dar es Salaam siku tatu kabla ya mapumziko ambayo yanamalizika leo.
DIMBA Jumatano lilivyozungumza na kocha wa kikosi hicho, Patrick Aussems, kujua sababu ya kuwa karibu na Ajib na pia kumpa majukumu ya kusambaza mipira wakati wa mazoezi ambapo alikiri kuona kitu cha ziada kutoka kwake.
“Tangu awali nilisema msimu huu nitatumia mifumo mitatu au miwili, kila mfumo una maana yake na ndiyo maana nataka kila mchezaji awe na uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja.
“Suala la upacha wa Ajib kucheza na Kagere kama washambuliaji wawili inawezekana ingawa Ajib si mshambuliaji asili, lakini bado anaweza kucheza pembeni ya Kagere akafanya vizuri sana,” alisema.
Ajib alifanikiwa kucheza dakika 10 za mwisho mchezo wa kwanza wa msimu mpya, Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya JKT Tanzani uliochezwa wiki iliyopita Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Ikumbukwe Ajib msimu uliyopita akiwa Yanga alikuwa akisimama nyuma ya Heritier Makambo, wakonekana kuwa mwiba mchungu kwa mabeki wa timu pinzani na kumfanya kutoa assist zaidi ya 10.
Msimu uliopita, safu ya ushambuliaji ya Simba iliyoongozwa na Kagere, Bocco na Okwi walifunga zaidi ya mabao 50 na kuwafanya kuibuka safu kali zaidi ya ushambuliaji kuliko ya timu yeyote.
Post a Comment