Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki wiki mbili kabla ya kukutana, kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema hata kama Ligi Kuu ya Zambia ni bora na nchi hiyo iko juu ya Tanzania kwenye viwango vya soka duniani, hilo haliwafanyi waingie kinyonge uwanjani kuivaa Zesco United.
Yanga itaikaribisha Zesco United ya Zambia katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaofanyika Septemba 14, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Endapo Yanga itashinda mechi zote mbili - nyumbani na ugenini dhidi ya timu hiyo, itatinga moja kwa moja hatua ya makundi ya ligi hiyo.
Zambia iko katika nafasi ya 81 kwenye viwango vya Shirikisho la Soka Dunini (Fifa), wakati Tanzania inashika nafasi ya 137.
Zahera alisema kama Simba waliichapa Al Ahly ya Misri, AS Vita ya Congo na JS Saoura ya Algeria haoni sababu kwa nini Zesco United waibuke wababe mbele zao.
Licha ya kukiri kuwa viwango soka vinatofautiana kati ya nchi na nchi, kocha huyo alisema haiwafanyi kuikabili Zesco kinyonge.
“Mpira wa Congo, Misri na Algeria ni mkubwa kuliko Tanzania, lakini Simba waliipiga Al Ahly, JS Saoura na AS Vita sasa Yanga itashindwaje kuifunga Zesco?” alihoji Zahera.
Msimu uliopita kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba iliichapa JS Saoura ya Algeria mabao 3-0, ikaifunga Al Ahly ya Misri bao 1-0 kisha ikaichapa AS Vita ya DR Congo mabao 2-1 na kutinga hatua ya makundi ya mashindano hayo.
“Hivi sasa tofauti ya mpira baina ya nchi na nchi si kubwa sana na licha ya Zambia kuwa ligi yao ni kubwa haitufanyi tuiogope Zesco. Tutacheza hiyo mechi tukiwa na lengo moja la ushindi na lazima tuhakikishe linatimia.”
Pia, Zahera alisema hana hofu na mechi hiyo licha ya kocha wa Zesco, George Lwandamina kuwahi kuifundisha Yanga kabla yake.
“Hata kama Lwandamina alipita Yanga hakuna tatizo wala hatuna hofu kwani mpira unabadilika. Sasa Yanga hii dhidi ya Zesco wao wana mipango yao na sisi tuna yetu, hivyo tutakutana uwanjani,” alisema.
Post a Comment