Katika michezo tisa ya ushindani ambayo wamecheza, Burundi wamepoteza minne kwa kufungwa na Guinea, Juni 30 kwa mabao 2-0, Juni 27 dhidi ya Madagascar kwa bao 1-0, Nigeria ambapo ilikuwa pia bao 1-0 kwenye fainali za mataifa ya Afrika ‘AFCON’.
Dar es Salaam. Washambuliaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, wakiongozwa na nahodha wao, Mbwana Samatta na Saimon Msuva wanatakiwa kukitumia vyema kipindi cha pili cha mchezo wa kuwania nafasi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia nchini Qatar 2022 dhidi ya Burundi, Septemba 4.
Stars itakuwa ugenini kwenye mchezo huo wa raundi ya kwanza utakaochezwa kwenye Uwanja wa Intwari, Bujumbura, Burundi kabla ya kurudiana nao, Jumapili ya Septemba 8 jijini Dar es Salaam.
Takwimu zinaonyesha kwamba tangu kuanza kwa mwaka huu, 2019, Burundi wamekuwa na udhaifu wa kuruhusu mabao mengi kipindi cha pili kuanzia dakika ya 61 hadi 75 na 76 hadi 90.
Katika michezo tisa ya ushindani ambayo wamecheza, Burundi wamepoteza minne kwa kufungwa na Guinea, Juni 30 kwa mabao 2-0, Juni 27 dhidi ya Madagascar kwa bao 1-0, Nigeria ambapo ilikuwa pia bao 1-0 kwenye fainali za mataifa ya Afrika ‘AFCON’.
Kipigo cha nne kilikuwa cha mabao 2-1, Juni 17, kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Tunisia ambao ulikuwa wa kujiandaa na AFCON, wametoka sare mbili, Juni 11 dhidi ya Algeria ya bao 1-1, ulikuwa mchezo wa kirafiki huku sare nyingine ikiwa ya bao 1-1 ambayo ilikuwa dhidi ya Gabon, Machi 23 kuwania nafasi ya kufuzu kwa AFCON, iliyofanyika nchini Misri.
Kati ya dakika ya 61 hadi 75, Burundi wameruhusu mabao matatu huku kuanzia ya 76 hadi 90 pia wakiruhusu mabao matatu kati ya tisa waliyofungwa mwaka huu.
Mabao hayo yalikuwa kwenye michezo dhidi ya Madagascar, Nigeria, Tunisia, Gabon, Algeria.
Udhaifu huo, uliopo kwenye kikosi cha Burundi unaweza kuwa faida kwa Stars kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mchezo huo ambao utawaweka kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele kabla ya mchezo wa marudiano Taifa.
Stars ndani ya mwaka huu, wamecheza michezo minane ya ushindani, ikiwemo mitatu ya fainali za mataifa ya Afrika nchini Misri, katika idadi hiyo, wameibuka na ushindi mara mbili, sare mbili na kupoteza michezo minne.
Michezo waliyoshinda ni dhidi ya Kenya, Agosti 4 kwa mikwaju ya penalti 4-1 katika kuwania nafasi ya kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika kwa wanaocheza soka kwenye ardhi ya nyumbani (CHAN) huku mwingine ukiwa Machi 24 dhidi ya Uganda waliowachapa 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa uliowapa tiketi ya kushiriki fainali za AFCON kwa mara ya pili. Taifa Stars imetoa suluhu mbele ya Kenya kwenye mchezo wa kwanza Julai 28, pia dhidi ya Zimbabwe ambapo ilikuwa sare ya bao 1-1 Juni 16, huku wakifungwa 3-0 dhidi ya Algeria Julai mosi katika mechi ya mwisho ya kundi lao la AFCON, pia Juni 27 ililala 3-2 dhidi ya Kenya wakati pia ilichapwa 2-0 dhidi ya Senegal katika ufunguzi wa kundi lao la AFCON Julai 23.
Mchezo wa nne kupoteza ulikuwa dhidi ya wenyeji wa AFCON kwa msimu uliopita, Misri ambao ulikuwa Juni 13 kwa bao 1-0, wakiutumia mchezo huo kama sehemu ya kujiandaa na fainali hizo.
Nguvu ya safu ya ushambuliaji ya Taifa Stars, inaonekana kuwa mwanzoni mwa kipindi cha kwanza, kuanzia dakika ya 46 hadi 60, katika dakika hizo kuna mabao mawili yamefungwa.
Mabao mengine manne yamefungwa kuanzia dakika ya 1 hadi 15, 16 hadi 30, 31 hadi 45 na 61 hadi 75.
Akikizungumzia kikosi chake, kaimu kocha mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije alisema wanaenda Burundi kucheza kwa kushambulia ili waibuke na ushindi kwenye mchezo huo licha ya kuwa ugenini.
“Mpira umebadilika siku hizi, unaweza kupoteza hata nyumbani, nina imani tunaweza kuvuka hii hatua kwa sababu nina kikosi kizuri chenye wachezaji wenye uzoefu wa soka la kimataifa,” alisema kocha huyo.
Nyota wenye uzoefu wa soka la kimataifa kwenye kikosi cha Taifa Stars mbali na wanaocheza soka la ndani ni Samatta (KRC Genk), Simon Msuva (Difaa), Himid Mao (Enppi), Ally Ng’anzi (Minnesota United), Farid Mussa (CD Tenerife), Adi Yusuph (Blackpool), Eliuter Mpepo (Buildcon), Hassan Kessy (Nkana) na Abdi Banda (Highland Parks) ingawa imeelezwa ameondolewa kikosini.
Katika wachezaji hao Samatta, Msuva na Adi wanadaiwa kuwa wataungana na wenzao nchini Burundi ambako utachezwa mchezo huo kwa mujibu wa kocha msaidizi, Juma Mgunda.
“Samatta, Msuva na Adi hao hawatokuja hapa, tutakutana nao Burundi. Wengine kwa asilimia kubwa wamewasili na tunaendelea nao na mazoezi,” alisema.
Upande wake Mpepo ambaye Jumamosi alikuwa akiichezea Buildcon mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Zambia ‘MTN’ dhidi ya Kabwe YSA, ametua jana, saa tisa za alfajiri akipitia Ethiopia.
Post a Comment