Uhamisho huo umemfanya Maguire ampiku Van Dijk, ambaye awali alikuwa akishikilia rekodi hiyo ya kuwa beki ghali duniani aliponaswa kwa Pauni 75 milioni miezi 20 iliyopita.
LIVERPOOL, England. LIVERPOOL inajianda kumpa ofa tamu Virgil van Dijk wakimpa mshahara wa kibosi zaidi huku ikidaiwa kwamba sababu kubwa ni Harry Maguire wa Manchester United.
Man United iliweka rekodi ya kumnasa Maguire kwa pesa ndefu na kuwa beki ghali zaidi duniani, walipomnyakua kwa Pauni 80 milioni akakipige huko Old Trafford.
Uhamisho huo umemfanya Maguire ampiku Van Dijk, ambaye awali alikuwa akishikilia rekodi hiyo ya kuwa beki ghali duniani aliponaswa kwa Pauni 75 milioni miezi 20 iliyopita. Lakini, sasa akiwa bora na cheo chake hicho amepokonywa, Liverpool wanatafuta namna nyingine ya kumfanya hadi ya Van Dijk kuendelea kuwa juu.
Wakati mkataba wake wa sasa ukiwa umebaki miaka minne na mshahara Pauni 125,000 kwa wiki, kuna dili tamu mezani, Liverpool wakitaka adumu kwenye timu yao huko Anfield kwa miaka sita zaidi na mshahara utakaokaribia Pauni 200,000 kwa wiki.
Jambo hilo litamfanya Mdachi huyo kuendelea kubaki Anfield hadi mwaka 2025. Baada ya kunaswa kwa pesa ndefu, Maguira ameripotiwa kulipwa mshahara wa Pauni 190,000 kwa wiki, hivyo Liverpool nao wanamtaka beki wao alipwe mshahara kama huo.
Van Dijk alikuwa mchezaji muhimu wakati Liverpool iliponyakua taji lao la sita la Ulaya na mwaka huu anapewa nafasi kubwa ya kubeba tuzo ya Ballon d'Or. Beki huyo wa zamani wa Celtic na Southampton, ameshabeba tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na ameingia kwenye tatu bora ya wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Fifa sambamba na Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.
Post a Comment