YANGA imepanga kuvaa pensi katika mchezo dhidi ya Zesco ili kumuunga mkono kocha wao Mwinyi Zahera aliyepigwa faini na Kamati ya Usimamizi ya Ligi Kuu kwa kosa la kuvaa mavazi yasiyo nadhifu.
Zahera amepigwa faini ya Sh 500,000 baada ya kuvaa pensi na fulana katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting uliofanywa Septemba 28 na kufungwa bao 1-0.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela amesema hawaoni kosa la kocha wao kwani kanuni haifafanui mavazi nadhifu ni yapi.
"Kwa tafsiri tunayojua sisi ya vazi nadhifu tunaona kocha wetu alivaa vizuri siku hiyo.
"Kama wachezaji, marefa, hata timu za Taifa wanavaa pensi kama alivyo kocha wetu sasa kwa nini yeye aadhibiwe?
"Tumeandika barua TFF (Shirikisho la Soka nchini) kuomba tafsiri sahihi ya vazi nadhifu ni nini na wasipotueleza mechi ijayo kocha anaava tena pensi"
"Sio kama sare hatuna, tunazo sana lakini hatujaona tatizo la kocha wetu kuvaa mavazi anayovaa kwani yuko safi tu na ili kumuunga mkono mechi ya Zesco United, wote kuanzia viongozi tunavaa kaptura na fulana kumuunga mkono kocha wetu," amesema Mwakalebela.
Pia Mwakalebela amesema wanaunga mkono kauli ya Zahera aliyoitoa baada ya mechi na Ruvu Shooting iliyosababisha afungiwe mechi tatu.
"Kocha wetu alizungumza kuwa sababu ya kupoteza mchezo wa Ruvu Shooting wachezaji walichoka, alikuwa sahihi kabisa hivyo hatujui kwa nini wamemfungia.
"Kabla ya mchezo huo tuliandika barua TFF, Bodi ya Ligi na hata Wizara ya Michezo kuomba mechi isogezwe kwani tulikuwa Botswana tuliondoka usiku baada ya mechi, timu isingeweza kufika alfajiri halafu kesho yake inacheza lakini hatukujibiwa.
"Tunaomba TFF wamuite kocha ili apewe nafasi ya kusikilizwa na kujieleza kwani hata sheria za nchi zinataka hivyo .Kama alivyozungumza vitakuwa uongo basi tutajua cha kufanya lakini tunavyojua kocha wetu ameonewa kwani aliongea ukweli na tunamuunga mkono," amesema.
Post a Comment