USHINDI wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, umemkuna Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussem, huku akiwamwagia sifa wachezaji wa timu hiyo, wakiwamo kipa Juma Kaseja na beki wa kati, Kelvin Yondani, akitamani wangekuwa ni wa kikosi chake.
Stars iliibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 3-0 dhidi ya Burundi katika mchezo wa kuwania kufuzu makundi ya kusaka tiketi ya fainali za Kombe la Dunia 2022 zitakazopigwa Qatar.
Katika mchezo huo wa juzi uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, hadi dakika 120 zinamalizika, timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1, kama ilivyokuwa katika mchezo wa kwanza wa Septemba 4, nchini Burundi, hivyo mshindi kuhitajika kupatikana kwa changamoto ya mikwaju ya penalti na Taifa Stars kushinda kwa matuta 3-0.
Shujaa wa mchezo huo, alikuwa ni Kaseja aliyeokoa penalti ya kwanza na nyingine mbili kwenda nje, huku Yondani akishirikiana na Erasto Nyoni kuwadhibiti washambuliaji wa Burundi waliokuwa wakiongozwa na straika anayekipiga Ulaya, Saido Berahino.
Akizungumza na BINGWA jana, Aussems alisema kuwa Kaseja na Yondani ni miongoni mwa wachezaji waliomkuna vilivyo, wengine wakiwa ni kocha wa Stars, Etienne Ndayiragije kwa kuwapa nafasi wachezaji wengine kadhaa kuonyesha uwezo wao.
Aussems alisema kikosi kilichocheza na Burundi ni tofauti na kile cha michuano ya Kombe la Mataifa Afrika, iliyofanyika Juni hadi Julai, mwaka huu nchini Misri ambapo timu hiyo ilikuwa chini ya kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike.
“Nimeangalia mechi mwanzo mwisho, naipongeza sana Taifa Stars, imefanya kazi nzuri, wachezaji wamejituma kwa kucheza katika kiwango cha juu, ukiangalia kuna utofauti wa kikosi hiki na kile kilichokwenda AFCON kutokana na uwepo wa nyota wapya,” alisema.
Alisema mbali ya Kaseja na Yondani, wachezaji wake wanaotoka Simba, wamemfurahisha zaidi, hasa Nyoni na Gadiel Michael kwa jinsi walivyoonyesha ujasiri wa kupiga penalti.
“Nimefurahishwa na wachezaji wangu wa Simba, wamefanya kazi nzuri, nimeona penalti za Gadiel na Nyoni, wamepiga kwa umakini mkubwa na kuisaidia timu kusonga mbele,” alisema.
Alipoulizwa iwapo angetamani Kaseja au Yondani kuwapo katika kikosi chake, alisema kuwa hakuna kocha anayeweza kukataa kuwa na mchezaji mzuri kikosini kwake.
“Ni wachezaji wazuri na walifanya vizuri, hakuna kocha anayeweza kumkataa mchezaji mzuri, lakini binafsi najivunia na wachezaji waliopo katika kikosi changu cha Simba, ni wazuri na wana uwezo wa kuwapa mashabiki matokeo mazuri,” alisema.
Nyota wengine wa Simba walikuwapo katika kikosi cha Stars kilichoivaa Burundi ni Jonas Mkude, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Beno Kakolanya ambaye alikuwa benchi.
Post a Comment