SASA ni rasmi kuwa, Ligi Kuu ya Uholanzi maarufu Eredivisie, msimu huu umefutwa kutokana na janga la corona.
Kufutwa kwa msimu huu wa 2019/20 wa ligi hiyo kumekuja ikiwa ni siku chache tangu serikali ya nchi hiyo kutangaza kusimamisha michezo hadi Septemba, mwaka huu.
Hatua ya kufutwa kwa msimu huu wa ligi hiyo kumekuja na uamuzi wa kutotambua bingwa wala timu ya kushuka daraja, hivyo vinara Ajax wamekosa kutetea ubingwa wao.
Pia wakati kukiwa hakuna bingwa wala timu ya kushuka daraja, upande mwingine hakuna timu itakayopanda daraja kutoka madaraja ya chini.
Mpaka ligi hiyo inasimama kutokana na janga la corona, Ajax ilikuwa kinara kwa tofauti ya mabao dhidi ya AZ Alkmaar iliyokuwa nafasi ya pili. Zote zilikuwa na pointi 56.
Hivyo basi, Ajax imetinga kucheza play-offs ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, wakati AZ Alkmaar ikianzia hatua ya pili ya kufuzu michuano hiyo na walioshika nafasi ya tatu, Feyenoord, wameingia moja kwa moja hatua ya makundi ya Europa League.
PSV na Willem II zenyewe zitacheza mechi za kufuzu kushiriki Europa League baada ya kukamata nafasi ya nne na tano.
Kwa wale waliokuwa mkiani, Fortuna Sittard, ADO Den Haag na RKC Waalwijk, wamepona, hawashuki daraja
Post a Comment