ARSTICA Cioaba, Kocha Mkuu wa Azam FC amewekewa mkataba mezani ili kubaki ndani ya klabu hiyo.
Awali kulikuwa na taarifa kuwa mabosi wa Azam FC wapo kwenye mpango wa kuachana na kocha huyo raia wa Romania ila kwa sasa mambo ni fresh.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Zakaria Thabith ‘Zaka za Kazi’ amesema kuwa kocha huyo ataendelea kusalia klabuni hapo kwani tayari washaanza taratibu za kumwongezea mkataba.
Mkataba wa Cioaba na Azam FC unatarajiwa kufikia tamati mwishoni mwa msimu huu huku ishu ya Corona ikionekana kuwa kikwazo katika dili hilo.
“Kwa kipindi kirefu sasa klabu yetu imekuwa na utaratibu wa kubadilisha makocha mara kwa mara kabla hata hawajamaliza msimu na kama unakumbuka vizuri kocha pekee wa Azam aliyewahi kumaliza msimu ni Stewart Hall, sasa tumefanya tathimini na kuona huo siyo utaratibu mzuri kwani unakuwa ni utaratibu unaolenga malengo ya muda mfupi.
“Sasa hivi tumeamua kubadilisha utaratibu na tunatamani kuona tunakuwa na mwalimu mmoja kwa kipindi kirefu, hivyo tumeanza kufanya utaratibu wa kumwongezea mkataba kocha Cioaba,” alisema Zakaria.
Cioaba ameiongoza Azam FC katika mechi 24 msimu huu na kukusanya pointi 45 baada ya kushinda mechi 13, amefungwa mechi tano na kutoa sare sita
Post a Comment