Nyota wa Kimataifa wa Tanzania, Saimon Msuva, anayekipiga katika timu ya Difaa El Jadid, inayoshiriki Ligi Kuu nchini Morocco, amefunguka na kuweka wazi kuhusiana na tetesi za usajili wake kuelekea Ulaya.
Baada ya kuwepo kwa tetesi zilizokuwa zikimuhusisha kutakiwa na Benfica ya Ureno na Panathnaikos ya Ugiriki, Msuva ameamua kuweka wazi juu ya sakata hilo na kuzungumzia hatma yake baada ya msimu huu kumalizika.
Akiwa nchini Morocco, Msuva ameliambia Gazeti la Championi kuwa ni kweli alitakiwa na Panathnaikos wakati wa kipindi cha dirisha dogo la usajili na alisaini nao mkataba wa awali (Pre-Contract) kwa ajili ya kujiunga na timu hiyo, lakini dili hilo lilikwama kutokana na kushindwa kufikia makubaliano baina yao.
“Ni kweli nilipokea ofa kutoka Panathnaikos na nilisaini nao mkataba wa awali lakini nilishindwa kwenda kwa sababu kuna baadhi ya vitu walishindwa kunitimizia mimi na rais wa klabu yangu, kwa hiyo nikashauriwa na rais wetu nisiende kutokana na timu hiyo kuyumba kiuchumi,” alisema Msuva.
Taarifa za Msuva kusaini Panathiakos na kupelekwa kwa mkopo Benfica lilizuia tafrani kubwa huku mwenyewe akiendelea kuwa kimya.
Hali hiyo ilisababisha mashabiki kuanza kulalamika wakidai walikuwa wamepewa taarifa ambayo si sahihi.
Hata hivyo, taarifa nyingine zinaeleza kuwa Msuva bado anatakiwa na klabu za Ulaya na hasa Ureno na Ugiriki na huenda akaondoka Morocco.
Msuva alijiunga na Difaa Al Jadida akitokea klabu ya Yanga ambayo aliichezea kwa mafanikio makubwa.
Post a Comment