Na Saleh Ally
ARSENAL ilikuwa klabu ya kwanza ya England kuruhusu wachezaji wake kuanza mazoezi kwa ajili ya mechi za kumalizia msimu ili kuanza na maandalizi ya msimu ujao.


Msimu wa 2019/20 umeingia matatizoni baada ya maambukizi ya Corona kuwa tishio la kuilazimisha dunia kusimama. Hadi sasa tayari watu zaidi ya 200,000 wamepoteza maisha duniani kote, bila ya ubishi hili si jambo la mchezo hata kidogo.


Pamoja na nguvu yake, michezo imelazimika kusimama ili kupisha adha hii ambayo hakika imeusumbua na inaendelea kuusumbua ulimwengu kwa kiwango cha juu kabisa.


Nchi za Ulaya ndio zimeathirika zaidi hadi sasa zikiongozwa na upande wa Bara la Marekani ya Kusini na hasa nchi ya USA.


Pamoja na yote, kama wanadamu mambo lazima yaendelee na maisha ili yasonge, vile vilivyosimama lazima viendelee na unaona hiki ndicho wanachojaribu kukifanya Ulaya licha ya kuwepo kwa hatari kubwa.


Ulaya wameanza kufanya utaratibu wa kurejesha ligi kuu mbalimbali za soka na unaona Ujerumani wamekuwa wa kwanza katika Bundesliga wakiwa wameanza mazoezi zaidi ya wiki sasa na matarajio ni kuanza kucheza mechi za ligi hiyo ifikapo Mei 9.


Wakati wao wameshapanga na tarehe, England ndio kama hivyo anao wameanza, Arsenal ikiwa ya kwanza lakini timu nyingine ikiwemo Tottenham nao wameanza mazoezi ikiwa ni harakati za kuhakikisha Ligi Kuu England inachezwa na kufikia tamati.


Unaweza ukaangalia jambo moja likawa lina mafunzo makubwa lakini tukaangalia jambo jingine likawa na mafunzo zaidi kwetu kupitia hawa wenzetu ambao kipindi hiki wanaanza kurejea.


Mwanzoni tu wakati Corona ndio imeingia na hapa nyumbani haikuwa ikisumbua au kutisha, wachezaji kadhaa wa Ligi Kuu England waliathirika baada ya kubainika wana virusi vya Corona.


Arsenal yenyewe ilipata tatizo hilo tena baada ya Kocha Mkuu, Mikel Arteta kuugua Corona. Sasa kocha huyo Mhispania anatarajia kuingoza Arsenal katika mazoezi baada ya kuwa amepona kabisa.


Aliyekuwa mgonjwa wa Corona atakwenda kazini, kuwafundisha wachezaji wake, jambo ambalo linaonyesha wenzetu wana uthubutu wa juu kabisa na haiwezekani wakaamua kufanya namna hii bila ya kuwa wamejiandaa.


Ukiangalia hadi jana mchana Uingereza waliokuwa wameathirika na Corona ni watu 157,147, kulikuwa hakuna hata mmoja aliyepona huku vifo vikiwa 21,092. Ujerumani walikuwa wameambukizwa watu 158,758 na waliopona ni 114,500 ambayo ni idadi kubwa zaidi duniani na vifo vikiwa ni 6,124.


Hapo ndio unaweza kujiuliza, kuwa hata kama Bundesliga au Premier League wanarejea kucheza bila ya mashabiki, kweli hii ni salama na hasa ukiangalia hatari ya ugonjwa wenyewe kwao?


Hawawezi wakawa wamekurupuka, lazima kuna jambo wanafanya na tayari baadhi tumeyaona ambayo ni kuhusiana na wachezaji kupimwa kwa kuwekwa karantini na zile tahadhari zitakazochukuliwa wakati wa mechi.


Wachezaji watakuwa wote chini ya uangalizi wa vyombo vinavyohusika na afya na si vibaya kusema maisha yao yatakuwa tofauti chini ya unagalizi lakini hili lote ni kutaka kumaliza ligi hizo wakiwa salama jambo ambalo wanaamini linawekana.


Nimezunguka kidogo lakini ninachotaka kusisitiza ni kwamba Ligi Kuu Tanzania Bara nayo ni vizuri tukifanikiwa kuiona inamalizika kwa ndiki hata kama mashabiki watakuwa hakuna.


Hivyo, wakati Ujerumani, England na kwingineko wanajaribu kuanza. Basi kuna kila sababu kwa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutegesha “kioo” nikimaanisha waanze kujifunza kutokana na kinachoafanyika sasa.


Kwa kuwa wao wakubwa ndio wanaanza, maana yake kuna nafasi kubwa ya kuona linalowezekana au lisilowezekana. Na kama tunaona wameweza basi ni vizuri kuanza kuangalia kwa kupitia aina ya mazingira yetu nini kifanyika.


Muda si mwingi wa kutosha sana, ikiwezekana wakati wanaanza, basi TPLB na TFF wanaweza wakaanza kujipanga kuangalia namna ambavyo itaruhusu mazoezi yaanze lakini katika ule mfumo wa tahadhari kubwa.


Kunaweza kukawa na changamoto za viwanja lakini kwa timu za Ligi Kuu Bara pekee, haziwezi kukosa sehemu sahihi za mazoezi kwa kipindi hiki ili wakati England, Ujerumani na kwingineko wanaendelea na TPLB na TFF wakijifunza, basi wachezaji nao wanakuwa wanajiandaa kama zoezi litawezekana.


Kikubwa ni elimu  kwa wachezaji kwa maana ya umuhimu wa kujikinga, mazoezi ambayo ikiwezekana yanaweza yakasimamiwa na wataalamu wa afya wakiangalia wapi sahihi na wapi la na kipi cha kufanya kwa usalama wakati wakisubiri TFF na TPLB wanachoangalia kuwa inawezekana kurejesha ligi bila mashabiki au la!


Kiuhalisia maisha lazima yaendelee, inawezekana Corona ni adui mpya lakini lazima kujipanga namna ya kupambana naye. Hivyo pale kunapokuwa na jambo zuri la kujifunza ambalo tunaweza kulifuata si vibaya ili kuendelea kupambana kwa kuchukua tahadhari lakini kuruhusu maisha yarejee.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.