NA SALEH ALLY
WAKATI huu michezo imesimama kwa ajili ya hofu ya maambukizi ya Covid 19, yaani ugonjwa wa homa ya mapafu ya Corona.
Ugonjwa huu ni hatari na ilikuwa sahihi kabisa kusimamisha michezo yote na kuwekeza nguvu zote katika kuhakikisha usalama wa afya unakuwa sawa.
Wakati haya yote tunayafikiria, wakati mwingine tena nimeona ninaweza kurudia kumzungumzia mdogo wake Said Hamis Ndemla, hii haiwezi kuwa mara ya kwanza au ya pili.
Unaweza ukashangazwa kwamba kwa nini sichoki na kwa nini ninaendelea lakini haya yote ni kwa kuwa ninaamini kiungo huyo ana kipaji na uwezo mkubwa na hautumiki sawasawa.
Ndemla amekulia katika timu ya vijana ya Simba, amekwenda taratibu anapanda hadi kufikia kuwa tegemeo la timu ya wakubwa na kama unakumbuka ile mechi ya mabao 3-3 dhidi ya Yanga ndiyo iliyomtangaza Ndemla na makocha na Wanasimba wakaanza kumuamini.
Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Simba, Abdallah King Kibadeni, miaka zaidi ya minne iliyopita alimuamini kumuingiza uwanjani katika mechi kubwa kabisa nchini Simba dhidi ya Yanga tena Simba ikiwa nyuma kwa mabao 3-0 na zimebaki dakika 45 tu!
Kibadeni aliamini Ndemla anaweza kuiokoa Simba iliyo nyuma kwa mabao matatu na ninaamini sote tuliona hakuwa amefikiri vizuri. Kwa kuwa alimtoa Haruna Chanongo na Abdulhalim Humud na kuwaingiza Ndemla na William Lucian maarufu kama Gallas na kweli wakaisaidia Simba kuikomboa ikipata sare ya mabao 3-3 na nusura ifunge bao la nne.
Mechi hiyo imebaki kuwa rekodi, historia na alama katika mpira wa Tanzania. Ajabu kabisa, hadi leo Ndemla bado anaendelea kubaki benchi na wakati mwingi jukwaani, binafsi inanishangaza sana.
Nani anamwambia Ndemla kubaki katika jukwaa la Simba ni bora zaidi kuliko kuichezea Mtibwa Sugar, kuliko kuichezea Kagera Sugar au kuliko kuichezea Azam FC au Coastal Union?
Kweli umri unamruhusu kwa sasa lakini haiwezi kuwa hivyo siku zote, anahitaji kujifurahisha pia kwa maana ya kuwa mpira ni furaha yake lakini anastahili kuzifikia ndoto zake na siamini zinaweza kuwa kukaa jukwaani au katika benchi la Simba na ikiwa hivyo, basi mimi ninayemshauri nitakuwa nakosea.
Ukiangalia kwa hesabu kwa sasa Simba ni kubwa zaidi ya Ndemla kwa kuwa watu wanaowaamini na kuwapa nafasi, wanaowataka wafanye kazi ya kuipigania Simba wengi zaidi ni viungo wa nje na wako kweli wenye kiwango bora.
Kiwango cha viungo hao ni kizuri lakini mimi bado sioni kinachomzuia kucheza mechi angalau 10 au zaidi kwa msimu kwa kuwa Simba inashiriki Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la Azam Sports lakini pia michuano ya kimataifa.
Kama Ndemla bado haaminiki licha ya kwamba aliaminika zaidi ya miaka minne iliyopita basi anapaswa kufunika tundu la mapenzi na aangalie mbele. Mapenzi aliyoonyesha Simba ni makubwa sana.
Huu ni wakati anastahili kuwa “profesheno”, yaani mtu anayeangalia kazi yake zaidi, mafanikio na namna ya kupita kuyapata. Kwa kweli bado kipaji cha Ndemla hakijatumika hata robo kutokana na kutopata nafasi ya kucheza na yeye kuamini ataendelea kusubiri hadi atakapoipata.
Angalia wengine wametoka wakarudi na kuwa na nafasi ya kucheza kuliko yeye na mfano mzuri ni Miraji Athumani. Lakini wako wamezunguka kwingi kama Hassan Dilunga, Ruvu, Yanga, Mtibwa Sugar leo wanacheza Simba, vipi Ndemla tu ndio ahofie na sote tunajua akiondoka Simba, wala hawezi “kupoteza maisha”!
Post a Comment