NA SALEH ALLY
NIMEMSIKIA beki Kelvin Yondani, maneno yake aliyoyasema wakati akifanya mahojiano na Gazeti la Spoti Xtra, hakika yanaonyesha nini maana ya ukongwe.


Yondani amemaliza ule ubishi kuwa anataka kuondoka, amemaliza kila kitu kuhusiana na yeye anabaki Yanga au la na amesema wazi kuwa ameamua kubaki Yanga hadi atakapostaafu soka.


Wazo hili linakuja akiwa sasa hana uhakika sana katika kikosi cha kwanza lakini unaona anachokizungumza ni mtu anayejielewa na anajua anafanya nini.

Yondani amesema hana mpango wa kuondoka Yanga na anajua kuendelea kubaki kwake inakuwa changamoto kwa maana ya kujituma na amesisitiza kwa wale ambao wataonekana wana nafasi, yeye kiroho safi kabisa atawapisha na kuwapa nafasi ya kufanya hivyo kwa maslahi ya Yanga.

Beki huyo aliyeanza kujulikana akiwa Simba, amesema amecheza timu zote kubwa ambazo ni Yanga na Simba na anaona hakuna sababu ya kuondoka Yanga kwa kuwa ndio sehemu amecheza kwa mafanikio zaidi na furaha.

Maneno haya ni matamu kuyasikia masikioni kwa mtu ambaye anakuzungumzia. Nimaamini kwa Wanayanga, maneno kutokea mwanzo hadi mwisho aliyozungumza Yondani yanapaswa kuwa yale yenye heshima kubwa na kuheshimiwa.

Mara nyingi nimekuwa nikiona wachezaji wengi hawapewi heshima kutokana na kile ambacho wamekifanya katika klabu zao wakati wakiwa katika kiwango kizuri cha cha kuvutia.

Hawapewi heshima kutokana na kiwango chao bora kilichoisaidia timu kubeba makombe na kufanya vizuri na kujenga heshima kubwa iliyokuwa ikikonga nyoyo za mashabiki.

 Ukizungumzia hayo, Yondani amefanya mengi sana makubwa ndani ya Yanga kuliko mchezaji yeyote yule aliye katika kikosi hicho kwa sasa. Msiangalie leo tu, kuwa nani alicheza vizuri katika mechi dhidi ya Simba au vinginevyo, fikirieni safari ya mchezaji akiwa na kikosi chenu.

Zaidi ya makombe matatu ya Ligi Kuu Bara, mara mbili au zaidi robo fainali ya michuano ya Caf na sote tunajua, Yanga bora ni ile ya kipindi ambacho Yondani akiwa katika kiwango chake, katikati anashirikiana na “chaboliii” yaani Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kusimamia ulinzi wa lango la Jangwani.

Makocha wote waliopita Yanga hakuna aliyewahi au kuthubutu kumuweka benchi, hata kama akifanya hivyo basi huenda kuna mgogoro. Yondani ni kati ya wachezaji walioivumilia Yanga kwa kiasi kikubwa sana huenda hata kuliko wengine wote walio katika kikosi hicho.

Wakati mwingine ilikuwa ikifikia anachoka na kuamua kususa lakini alikuwa na haki kama mwanadamu kwa kuwa alifanya hivyo baada ya ahadi nyingi licha ya uvumilivu wake wa kiwango cha kupitiliza.

Yondani amekuwa mhamasishaji wa wenzake kuhakikisha wanaendelea kupambana, mkali kwa wale wanaozembea wakati Yanga inapotaka kudidimia na hakuna ubishi bado ana rekodi ya kuwa mmoja wa mabeki bora kabisa wa kati katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa sasa ndio anaingia ukingoni sababu ya kitu kimoja tu, umri! Huu hakuna ambaye amewahi kushindana nao na akaushinda, kutakuwa na afadhali tu lakini  hauwezi kuwa na uwezo wa kucheza ukiwa na miaka 30 na zaidi halafu ikawa sawa na kama ulivyokuwa na umri wa miaka 18 au 22. 

Kawaida mchezaji anapokuwa anakwenda ukingoni anakosa mambo kadhaa kama uwezo wa kuamua haraka, kasi inapungua, nguvu pia inapungua. Hivyo hawezi kuwa yule mliyemzoea.

Lile neno “ameisha”, limekuwa likitumika vibaya bila ya kufikiria na hasa hapa nyumbani. Vizuri tukaiga angalau wenzetu Ulaya unaona shabiki anakuwa anajua fulani katenda mengi na leo ni kiwango tu kinashuka kutokana na umri lakini anastahili heshima si kwa ajili ya leo pekee badala yake kote tulipopita naye.

Yondani ni Legend ndani ya Yanga, ameamua “kufia” Yanga, basi “kufeni” naye na muonyesheni heshima kwa kuwa ameonyesha wazi namna anavyoiheshimu na kuithamini Yanga. Kwa wale ambao hamkumjua mapema na huenda mnahadithiwa tu, basi mnaweza kumpa heshima kutokana na hayo mnayoyasikia badala ya kuamini ukiwa shabiki, basi una haki ya kumdharau yeyote unavyotaka wewe hata kama anastahili heshima kutokana na nguvu na maisha yake aliyoweka katika klabu yenu. Sisi sote ni wanadamu, tunaelewa nini maana ya umri mkubwa, hivyo tubadilike na kuwapa heshima wale wanaofikia umri unaoweza kuwazuia kufanya yale ambayo mgependa yatokee

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.