IMEFAHAMIKA kuwa jina la kiungo mkabaji wa Mtibwa Sugar, Abdulhalim Humoud ‘Gaucho’ ndiyo limemuondoa Said Ndemla kwenye orodha ya majina ya usajili yaliyopendekezwa na Kamati ya Usajili ya Yanga.
Awali, yalikuwepo majina mawili ya viungo wakabaji wazawa yaliyokuwa yakijadiliwa na kati ya hilo lilikuwepo na Ndemla ambaye mkataba wake na Simba unatarajiwa kumalizika mwisho mwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara.
Humud ilielezwa kuwepo na mazungumzo ya siri na kocha mkuu wa timu hiyo, Luc Eymael baada ya kuvutiwa na kiwango chake wakati Yanga ilipocheza mchezo wa ligi na Mtibwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mtoa taraifa huyo alisema kuwa sababu iliyomuondoa Ndemla ni kutokana na kutocheza katika kikosi cha Simba tofauti na Humud ambaye ni tegemeo katika timu yake ya Mtibwa.
“Mara kadhaa Yanga ilikuwa ikionekana kumuhitaji Ndemla, lakini yeye alionekana kuonyesha nia ya kuendelea kubaki Simba licha ya kutokuwa na nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza kwa misimu yote aliyokuwepo hapo.
“Msimu huu anaonekana mwenyewe anataka kuja Yanga, ni baada ya kuona Simba haina mpango naye hivyo baadhi ya viongozi wameliondoa jina lake na kuliingiza la Humud ambaye ameonekana kuonyesha nia ya kuichezea Yanga.
“Humud uwezo wake kocha ameshaukubali baada ya kumuona tulipocheza na Mtibwa, yeye alionekana kikwazo kwetu kutokana na kufanikiwa kupunguza mashambulizi na kuokoa hatari golini kwao,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassani Bumbuli kuzungumzia hilo alisema kuwa “Usajili bado haujaanza licha ya kuwepo mapendekezo kadhaa ya kocha ambayo ameyatoa na kuyakabidhi kwenye Kamati ya Utendaji ya Yanga ambayo ni siri, hivyo huenda hilo jina likawepo.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, Ndemla ambaye amekuwa akihusishwa na Yanga mara kwa mara ameondolewa kwenye mipango hiyo ya kusajiliwa na Humud ndiyo amepewa nafasi hiyo kwa kiungo mkabaji huku kocha Eymael akipanga kumleta mwingine kutoka nje ya nchi.
Post a Comment