NYOTA anayekipiga ndani ya Klabu ya Mtibwa Sugar, Salim Kihimbwa inaelezwa kuwa yupo kwenye hesabu za wakali wa Kagera Sugar na Yanga ambao wanawania kuinasa saini yake kwa ajili ya msimu ujao.
Kihimbwa amekuwa kwenye ubora wake msimu huu licha ya kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara ndani ya uwanja kwani alipata dili la kufanya majaribio nje ya nchi ambalo limetibuka kutokana na maambukizi ya Virusi vya Corona.
Kwa sasa Ligi Kuu Tanzania Bara imesimamishwa kutokana na maambukizi ya Virusi vya Corona ambapo wachezaji wapo nyumbani wakiendelea kufanya mazoezi binafsi pamoja na kuchukua tahadhari dhidi ya Corona.
Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema kuwa wamekuwa wakifuatilia wachezaji wote ndani ya Ligi Kuu Bara ili wakati wa usajili ukifika wasipate tabu.
"Tunafuatilia kila mchezaji ndani ya Ligi Kuu Bara pamoja na wale ambao hawapo kwenye Ligi Kuu Bara yaani wale wa Daraja la Kwanza, masuala ya usajili wakati wake haujafika," amesema.
Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru amesema kuwa kwa sasa muda wa kuuza wachezaji bado na nguvu nyingi wameziwekeza kupambana na Virusi vya Corona.
"Tumewaambia wachezaji wawe mabalozi, masuala ya usajili hatuwezi kuzungumza tunapambana na Corona," amesema
Post a Comment