WASHAMBULIAJI wa Yanga, Maybin Kalengo na Issa Bigirimana, wamekiona cha moto kutoka kwa kocha wao, Mwinyi Zahera, aliyewahenyesha vilivyo katika mazoezi ya juzi na jana ili kuwapa makali zaidi.
Wawili hao waliotua Yanga hivi karibuni, wameonekana kutokuwa na makali yaliyotarajiwa tofauti na ilivyo kwa wenzao kama Patrick Sibomana, Juma Balinya, Sadney Urikhob na wengineo.
Katika mazoezi ya timu hiyo yanayoendelea mjini Morogoro, Bigirimana na Kalengo ambaye alikuwa akiandamwa na jeraha la enka, wamekuwa wakidorora, kama walivyojionyesha katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Mawenzi Market uliopigwa Uwanja wa Chuo cha Biblia, mjini humo, mapema wiki hii.
Ni kutokana na kubaini hilo, juzi na jana, Zahera aliamua kuwafungia kazi ili kuwapa makali yaliyotarajiwa na wapenzi wa Yanga.
Katika mazoezi ya juzi, Zahera aliwatenga wawili hao na wenzao na kuwapa maoezi ya nguvu, huku mara kwa mara akizungumza nao.
Wakati huo huo, katika kuelekea kilele cha Wiki ya Wananchi, kikosi cha Yanga pamoja na viongozi wao, wamewafariji wagonjwa wa hospitali ya Mkoa wa Morogoro ambapo waliwasalimia na kuwapa zawadi mbalimbali.
Kilele cha Wiki ya Wananchi kinatarajiwa kufanyika Jumapili hii kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Kariobang Shark ya Kenya, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Post a Comment