ONESMO KAPINGA

SIMBA imetolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya UD Songo ya Msumbiji, katika mchezo uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Wekundu wa Msimbazi hao wameaga michuano hiyo baada ya kupata suluhu katika mchezo wa kwanza uliopigwa nchini Msumbiji wiki mbili zilizopita.

Hata hivyo, kutolewa kwa Simba katika michuano hiyo, kumepokewa kwa hisia tofauti na wapenzi wa klabu hiyo, baadhi wakidai kitendo hicho kimechangiwa na kutemwa kwa James Kotei, lakini pia kuondoka kwa Emmanuel Okwi.

Kama hilo halitoshi, jina la Ibrahim Ajib nalo lilitajwa na mashabiki wa Simba baada ya mchezo huo jana, wakidai ametua Msimbazi na gundu akitokea Yanga.

Wakizungumza kwa hasira wakati wakitoka uwanjani baada ya mchezo wa jana, mashabiki hao walikuwa wakisema inashangaza pamoja na kuwa na kikosi kizuri, wametolewa kirahisi, tena wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani.

“Hapa si bure, kuna kitu…haiwezekani kikosi kama hiki, tunatolewa kirahisi hivi. Huyu Ajib inawezekana ni tatizo, alipokuwa Yanga timu yao haikuwa ikifanya vizuri, amekuja huku (Simba), tumetolewa,” alisikika mmoja wa mashabiki hao akisema.

Kwa upande wake, mmoja wa viongozi wa Simba ambaye hakutaka jina lake kuwekwa wazi, alisema: “Wakati wa usajili, niliwaambia Kotei asiachwe, ni mtu muhimu, lakini kuna watu wakajifanya wajuaji.

“Leo tumeona pengo lake, lakini pia kuondoka kwa Okwi kumechangia, Kagere (Meddie) kusimama peke yake pale mbele ni tatizo, alipokuwa na Okwi alikuwa na madhara zaidi kwa kuwa Okwi alikuwa akiwasumbua sana mabeki na kutoa nafasi kwa Kagere kufunga.”

Alisema pamoja na usajili wa wachezaji wapya kama Sharaf Shiboub, Deo Kanda, Francis Kahata na wengineo, bado Kagere anatakiwa kupata mshambuliaji wa kusaidiana naye mwenye makeke kama Okwi.

Katika mchezo wa jana, ulichezeshwa na mwamuzi Jean Claude Isimwe kutoka Rwanda, UD Song ndio walioanza kuichachafya Simba kwa kufanya mashambulizi mawili mfululizo dakika ya tatu kupitia kwa mshambuliaji wao, Luis Miquissone, lakini hayakuzaa matunda.

Simba walijibu mapigo dakika ya 11 baada ya kufanya shambulizi kali, lakini Kahata alishindwa kuitendea haki pasi ya mwisho ya Shiboub baada ya shuti lake kuokolewa na mabeki wa UD Song.

Makosa yaliyofanywa na Shomari Kapombe ya kumfanyia faulo Stelio Ernesto nje ya 18, yaliiwezesha UD Song kuandika bao la kuongoza dakika ya 13 lililofungwa na Miquissone kwa shuti la moja kwa moja.

Simba walifanya shambulizi la nguvu dakika ya 26, lakini Kahata alishindwa kuunganisha nyavuni pasi murua ya Kagere.

Baadaye, Simba walifanya shambulio lingine dakika ya 30, baada ya Kanda kuwatoka mabeki wa UD Song na kutoa pasi murua kwa Clatous Chama aliyekuwa katika nafasi nzuri ya kufunga, lakini akashindwa kufanya hivyo.

Iwapo washambuliaji wa Simba wangekuwa makini dakika ya 44, wangeweza kupata bao la kusawazisha, lakini walijibabatiza wenyewe kwa wenyewe na mabeki wa UD Songo kuondosha hatari hiyo na kuwa kona tasa.

Kwa ujumla, dakika 45 za kwanza, UD Song walionekana kutawala mpira, huku mabeki wa Simba kupata shida kumkaba Miquissone aliyekuwa mwiba mchungu kwa Wekundu wa Msimbazi hao.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi baada ya Simba kukosa bao dakika ya 46 baada ya shuti kali la Gadiel Michael kupanguliwa na kipa wa UD Songo, Leonel Pendula.

Kagere alikosa bao la wazi baada ya kupiga shuti lililopaa akiwa ndani ya sita, akipokea krosi murua kutoka kwa Gadiel.

UD Song almanusura waandike bao la pili dakika ya 63 baada ya John Banda kupiga shuti kali na kipa wa Simba, Aishi Manula kudaka.

Beki wa Simba, Erasto Nyoni, aliisawazishia timu yake bao kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa baada ya beki wa UD Song, Hermenegil Do Mutambe, kumwangusha Miraji Athuman katika eneo la hatari.

Baada ya mchezo huo, Kocha wa Simba, Patrick Aussems, amesema wachezaji wake hawakucheza vizuri kipindi cha kwanza, ndio maana walishindwa kushinda mchezo huo.

Alisema malengo yao ya kufika mbali Ligi ya Mabingwa Afrika, hayajatimia baada ya msimu uliopita kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Aussems amewataka mashabiki wa Simba kutulia wakati wakijipanga kuandaa kikosi bora, akiapa kumaliza hasira zao zote Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kutoa kipigo kwa kila timu watakayokutana nayo.

SIMBA: Aishi Manula, Gadiel Michael/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ (dk 77), Shomari Kapombe, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Deo Kanda, Sharaf Shiboub/Miraji Athumani (dk 62), Meddie Kagere, Clatous Chama na Francis Kahata/Hassan Dilunga (dk 42).

UD SONG: Leonel Pendula, Antonio Chirinda, Infren Matola, Pascoal Carlos, Hermenegil Do Mutambe, Amade Momade, John Banda, Luis Miquissone, Pachoio King, Stelio Ernest/Mario Sinamunda (dk 68) na Frank Band/Cremildo Nhantumbo (dk 56).

Tags:

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.