Wachezaji hao ni beki Ally Ally; viungo Feisal Salum, Abdulaziz Makame, Deus Kaseke na Raphael Daud pamoja na washambuliaji Maybin Kalengo na David Molinga.
Dar es Salaam. Wachezaji saba wa Yanga wamejiweka kwenye nafasi ngumu ya kupata namba katika kikosi cha timu hiyo kitakachocheza mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ugenini dhidi ya Township Rollers ya Botswana, wiki ijayo.
Kiwango kisichoridhisha na ufanisi mdogo wa wachezaji hao kwenye mechi za hivi karibuni zile za kirafiki, vinaweza kuwakaanga na kujikuta wakisotea benchi. Na si mechi hiyo tu, bali hata zile za mashindano mengine wanaweza kujikuta wakikosa namba.
Wachezaji hao ni beki Ally Ally; viungo Feisal Salum, Abdulaziz Makame, Deus Kaseke na Raphael Daud pamoja na washambuliaji Maybin Kalengo na David Molinga.
Makosa ya washambuliaji Molinga na Kalengo kushindwa kutumia nafasi ambazo Yanga ilitengeneza na pia hata wao wenyewe kutopika mabao kwa wengine, vinawaweka kwenye wakati mgumu kuwapora nafasi Juma Balinya na Sadney Urikhobi.
Katika mechi zote za kirafiki ambazo zimeonekana kuwa za ushindani, Kalengo na Molinga wameshindwa kupachika mabao.
Pia hali inaweza kuwa tete kwa viungo Kaseke, Makame, Feisal na Daud kutokana na kushindwa kutimiza vyema majukumu yao kwenye safu hiyo ambayo ni kiunganishi cha timu kinachotengeza nafasi za mabao. Kukosa ubunifu na kutengeneza muunganiko wa kitimu utawapa kazi ya ziada kulishawishi benchi la ufundi kuwapatia nafasi mbele ya Mapinduzi Balama, Patrick Sibomana, Pappy Tshishimbi na Mohamed Issah ‘Banka’.
Na kwa kuthibitisha ugumu wa wachezaji hao kupata nafasi kwenye mechi ya marudiano dhidi ya Rollers na hata za mashindano mengine, kocha Mwinyi Zahera ametumia mechi mbili za kirafiki dhidi ya Polisi Tanzania juzi, na ile ya Malindi wiki chache zilizopita kama mfano halisi.
“Hii ni klabu kubwa. Mchezaji unapopata nafasi unapaswa kuonyesha kama unachezea timu kubwa. Mfano leo (juzi) dhidi ya Polisi Tanzania nimefanya mabadiliko ya kikosi ili kuwapa nafasi ya kucheza, lakini wameshindwa kuitumia,” alisema Zahera baada ya timu hiyo kupokea kichapo cha maba 2-0 kutoka kwa Polisi Tanzania mjini Moshi.
Post a Comment