IILINICHANGANYA kidogo wakati Simba walipoachana na beki wao wa kulia, Zana Koulibaly aliyetua kwa mbwembwe msimu uliopita. Alianza kwa kuboronga, akaonekana mzito. Kadiri siku zilivyosonga mbele watoto wa mjini wakasema ‘Gari limewaka’.
Baadaye akawa mchezaji muhimu. Mechi nyingi muhimu za CAF akacheza. Mwishoni mwa msimu akaachwa na akaenda AS Vita ya Congo. Ilinidhanganya kidogo. Vita waliona nini kwa Coulibaly? Mchezaji ambaye Simba hawakuamini kwamba angewafaa msimu huu alichukuliwa na Vita, moja kati ya klabu bora na kubwa Afrika.
Nikakumbuka kwamba beki wa kulia wa Simba, Shomari Kapombe alikuwa mbioni kurudi kutoka katika majeraha. Shomari ni beki bora zaidi wa kulia wa zama hizi. Nikawaza, ina maana Shomari ni bora kuliko Koulibaly? Jibu ni ndio. Bora kwa mbali zaidi.
Nikakumbuka kwamba kilichomrejesha Shomari nchini kilikuwa ni uzembe fulani tu. Klabu ya Caen ilimuweka afanye mazoezi pale kwao wakati akipikwa kumudu soka la Ulaya. Sijui ilikuwaje akarudi. Ninachojua leo hii Shomari angekuwa mmoja kati ya mabeki bora wa pembeni Ulaya. Angeweza kutoka katika soka la Ulaya kabla ya Mbwana Samatta.
Hii ilinikumbusha kwamba tunawapokea wachezaji wengi wa kigeni kutoka nje, tunawalipa pesa nyingi, lakini mwisho wa siku tuna wachezaji bora wa ndani kuliko wageni. Lakini hapa hapa unawaza jinsi ambavyo kina Shomari walivyozembea kuwa hapa.
Simba inaweza kuachana na mchezaji wa kigeni atakayegombewa na Vita kwa ajili ya kupewa jeuri na beki wa kizawa. Inafurahisha moyoni. Lakini hapo hapo inatia simanzi tunapokumbuka kwamba hata hawa wageni ambao wanatamba leo wanacheza nafasi hizi kwa sababu ya uzembe wa wazawa tu.
Katika kisa hivi cha Shomari na Koulibaly unakumbana na kisa cha Asante Kwasi na Mohamed Hussein ‘Tshabala’. Nini kimetokea? Kwasi ambaye ni Mghana ameachwa na amekwenda Baroka ya pale Afrika Kusini. Wakati tukiwaza kwamba ‘Tshabalala’ siku moja acheze Ligi Kuu ya Afrika Kusini kumbe ana uwezo wa kumsugulisha benchi mchezaji staa wa kigeni ambaye ataonekana mali katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Hii ina maana Tshabalala ana uwezo wa kucheza Baroka bila ya shida. Au Utanzania wake ungeweza kuwa shida? Lakini tukumbuke Abdi Banda alicheza pale kiasi cha kufikia kupewa unahodha. Inachanganya kidogo.
Ina maana Tshabalala angeweza kucheza Baroka, kisha akaonyesha kiwango kizuri halafu angenaswa na timu kubwa zaidi ya Baroka. Nini kinamtokea? Labda hana njia za kutoka. Mpira wa Afrika Kusini unalipa vizuri kuliko wa nyumbani.
Lakini hapo hapo linajitokeza jambo jingine. Inawezekana Simba kwa sasa imekuwa timu kubwa kuliko Vita na Baroka. Inawezekana. Labda Simba itolewe mapema katika hatua hii lakini kwa kufuatilia takwimu za msimu uliopita basi Simba ni timu kubwa kuliko Vita na Baroka. Kwamba zinaweza kumuona mchezaji hafai halafu ‘akaokotwa’ na klabu hizo.
Lakini hapo hapo kuna jambo jingine ambalo limejificha ndani yake. inawezekana Simba haikujua kuwatumia mastaa hao na huenda baada ya muda mfupi Simba ikaumbuka. Hilo nalo lipo lakini ina tafsiri pana zaidi.
Kwa mfano, Laudit Mavugo alionekana hafai Simba lakini amekuwa mfungaji bora katika Ligi Kuu ya Zambia. Katika ligi ngumu yenye wachezaji mafundi kama Zambia inakuaje yule ‘Mchovu’ Mavugo aibuke kuwa mfungaji bora? Mpira wetu una matatizo au mpira wa Zambia una matatizo.
Itakuwaje kama Kwasi akichaguliwa kuwa mchezaji bora katika kikosi cha Baroka msimu ujao?
Tutaweka wapi sura zetu? Kama akiitwa katika kikosi cha Timu ya Taifa ya Ghana ambayo wakati mwingine huwa inaangalia wachezaji kutoka Afrika Kusini tutaweka wapi sura zetu?
Hawa wachezaji wetu, Koulibaly na Kwasi wameacha maswali mengi ya msingi. Naendelea kuamini kuwa tuna wachezaji wengi wa ndani wenye uwezo kuliko wachezaji wa kigeni lakini hawachezi kwa asilimia 100. Shomari na Tshabalala wanacheza kwa asilimia 100 na wamewang’oa wageni mahiri katika nafasi zao.
Ni kama ninavyoamini hawa kina Meddie Kagere wanang’ara kwa sababu zama za kina Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ zimepita. Angecheza wapi mchezaji anayeitwa Sibomana kama angemkuta Edibily Lunyamila katika ubora wake? Labda Shomari na mwenzake wametuonyesha kwamba tukicheza soka la asilimia zote na kujituma hatuhitaji sana wachezaji wa kigeni.
Koulibaly na Kwasi wamenifikirisha kwa maswali mengi ambayo hayana majibu. Kama Simba imechukua uamuzi sahihi kuhusu wao basi nadhani kuna umuhimu wa kuanzisha mjadala kuhusu wachezaji wetu wa ndani. Naamini wanatoa ruhusa kubwa ya wageni kutamba.
Pengine hili si la uongozi wa TFF wala klabu zao. Pengine wajitakafari zaidi.
Kwanini Simba wamemuamini zaidi Shomari kuliko Koulibaly aliyecheza mechi nyingi?
Post a Comment