Fowadi huyo wa Kibelgiji aliachana na miamba hiyo ya Old Trafford na kutua zake San Siro kwa ada ya Pauni 73 milioni kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi na kuwarushia madongo klabu yake ya zamani.
Milan, Italia. STRAIKA wa Inter Milan, Romelu Lukaku amesema kwamba yeye, Paul Pogba na Alexis Sanchez walifanywa mbuzi wa kafara tu kwenye kikosi cha Manchester United msimu uliopita.
Fowadi huyo wa Kibelgiji aliachana na miamba hiyo ya Old Trafford na kutua zake San Siro kwa ada ya Pauni 73 milioni kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi na kuwarushia madongo klabu yake ya zamani.
Lukaku alisema ilibidi tu kukubaliana na kila kitu kuhusu kukosolewa kwa kipindi alichokuwa kwenye kikosi cha Man United hasa kwenye mwaka wake wa mwisho katika timu hiyo ya Old Trafford.
Alisema: "Ilikuwa lazima watafute mtu. Ilikuwa Pogba, mimi au Alexis. Ni sisi watatu kila wakati. Mimi nilikuwa nalitazama hilo katika njia nyingi."
Pogba kiwango chake cha ndani ya uwanja kilikuwa kikipanda na kushuka, wakati Sanchez kwa msimu wote alifunga mara moja kwenye Ligi Kuu England.
Straika Lukaku hakuifungia tena Man United tangu alipofunga mara mbili kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Paris Saint-Germain, Machi 6 na baada ya hapo alicheza mechi nane akitoka patupu.
Lakini, kwenye mechi mbili za kufuzu Euro 2020 akiwa na Ubelgiji dhidi ya Kazakhstan na Scotland zilizochezwa wiki sita baada ya kucheza mechi yake ya mwisho huko Man United, Lukaku alifunga mabao matatu.
"Hivi vitu vilikuwa vinanichekesha sana, inakuwaje mbaya kwenye klabu yangu, lakini ninapocheza timu ya taifa nakuwa mzuri? Nafurahi tu," alisema Lukaku. Man United ilimnasa Lukaku kutoka Everton kutoka mkwanja wa Pauni 75 milioni, lakini imemuuza baada ya miaka miwili tu.
Post a Comment