NA ZAINAB IDDY
LIGI Kuu Tanzania Bara msimu wa 2019/20 inaanza leo, huku jina la Abdallah Kambuzi kutoka Shinyanga likitolewa katika orodha ya waamuzi watakaocheza mechi za Ligi Kuu mzunguko wa kwanza.
Kambuzi ameondolewa katika orodha ya waamuzi msimu huu kutokana na rekodi yake ya kushindwa kutafsiri sheria 17 za soka mara kwa mara katika mechi zalizopewa ‘rungu’ misimu iliyopita.
Mathalan, msimu uliopita, Kambuzi alifungiwa baada ya kukutwa na tuhuma za kuwapa penalti isiyo halali vijana wa Simba, zikiwa zimebaki dakika chache kabla ya kumalizika kwa mchezo wao dhidi ya KMC katika Uwanja wa taifa, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa orodha ya waamuzi watakaochezesha mechi za mzunguko wa kwanza ambayo BINGWA limeipata, Ludovick Charles ataamua mchezo kati ya Alliance FC dhidi ya Mbao FC utakochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Katika mchezo huo, Charles atasidiwa na Frednand Chacha na Josephat Masija, huku kamisaa wa mchezo akiwa ni Frank Chavala, wote kutoka Mwanza.
Mchezo kati ya Mbeya City dhidi ya Tanzania Prisons itakayochezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya, mwamuzi wa kati ni Fiorentina Zabron atakayesaidiwa na Charles Simon, wote wa Dodoma, wakati msaidizi namba mbili ni Credo Mbuya na Kamisaa ni Mashaka Mwandembwa wa Mbeya.
Huko Mkoani Mara, mchezo kati ya Kagera Sugar dhidi ya Biashara United utaamuliwa na mwamuzi Meshack Sudi, atakayesaidiwa na Athuman Rajabu na Sudi Hussen (Kigoma), wakati Kamisaa wa mchezo ni Francis Azaria (Mara).
Mechi kati ya Mwadui dhidi ya Singida United itakayochezwa CCM Kambarage, Shinyanga, itaamuliwa na mwamuzi Jonesia Rukyaa akisaidiwa na Grace Wamala na Edger Lyombo wote kutoka Kagera, wakati Kamisaa atakuwa ni Makame Mdogo wa Shinyanga.
Mechi ya mwisho itakayochezwa leo ni ile ya Polisi Tanzania dhidi ya Coastal Union itakayochezwa Uwanja wa Ushirika, Moshi, mpuliza kipenga akiwa ni Emmanuel Mwandemba, akisaidiwa na Robert Ruhemeje na Abdulazizi Ally (Arusha), huku kamisaa akiwa ni Crispin Mwakalinga (Kilimanjaro).
Post a Comment