Dar es Salaam. Wakati Simba ikiaga mashindano ya kimataifa, Kocha wa UD Songo Chaquir Bemate, amefichua siri ya kuing’oa timu hiyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba ambayo msimu uliopita ilifika robo fainali, imeungana na KMC iliyochapwa mabao 2-1 dhidi ya AS Kigali ya Rwanda na KMKM iliyopigwa jumla ya mabao 3-0 dhidi ya Agosto ya Angola kuaga mashindano hayo. Simba jana ilitoka sare ya bao 1-1.
Akizunguza Dar es Salaam, jana, Bemate alisema walitumia udhaifu wa mabeki wa kati Erasto Nyoni na Pascal Wawa kupata ushindi huo.
Alisema mabeki hao hawana kasi na waliwasoma katika mchezo wa awali waliotoka suluhu mjini Maputo, Msumbiji wiki mbili zilizopita.
“Tulitumia udhaifu wa mabeki wa kati kupitisha mipira yetu kwasababu tangu mechi ya kwanza tulibaini wanacheza taratibu sana,” alisema.
Kocha wa Simba, Patrick Aussems alisema wamekosa ushindi kwa kuwa washambuliaji wake walishindwa kumalizia pasi za mwisho.

Aussems alisema licha ya kutengeneza idadi kubwa ya nafasi, wachezaji hawakuwa watulivu walipoingia ndani ya eneo la hatari.
“Nimeridhika na kiwango cha timu hasa kipindi cha pili tuliwabana vizuri lakini tulikosa bahati ya kuweka mpira wavuni,” alisema Aussems.
Kipindi cha Kwanza
UD Songo ilianza mchezo kwa kasi na dakika nane za kipindi cha kwanza ilitawala.
Kitendo cha US Songo kushambulia kwa kasi kilikuwa kikwazo kwa mabeki wa Simba, ambao walikuwa na kazi ya ziada kupunguza kasi ya mashambulizi.

UD Songo ilitumia mfumo wa kufunguka tofauti na Simba ambayo ilitegemea wapinzani wao wangecheza mchezo wa kujilinda.
Francis Kahata na Jonas Mkude waliocheza kiungo, walishindwa kulisha mipira kwa kina Meddie Kagere na  Clatous Chama licha ya Deo Kanda kusukuma mashambulizi mbele.
UD Songo ilipata bao la kuongoza dakika ya 13 lililofungwa na nahodha Luis Misquissone.
Haikushangaza Aussems kumtoa Kahata na kumuingiza Hassani Dilunga licha ya kubaki dakika tano kabla ya timu hizo kwenda mapumziko.

Kipindi cha Pili
Dakika ya 70 Simba ilifanya shambulio kupitia kwa Kanda aliyepokea pasi ya Mkude lakini alipiga kiki iliyopanguliwa na kipa Leonel Pendula. Dakika ya 84 Simba ilipata bao kwa mkwaju wa penalti uliopigwa na Nyoni, baada ya Miraji Athumani kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari.

Kauli za Wadau
Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella alisema kipigo hicho ni pigo kubwa kwa timu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi.
Mogella alisema Simba imevuna ilichopanda kwani ilikuwa na maneno mengi na kusahau kufanya maandalizi ya kutosha.
“Kujiamini na maneno mengi vimetuponza na kusahahu mpira hautaki maneno bali vitendo, tulitarajia usajili wa msimu huu utusaidie lakini imekuwa tofauti, Yanga sikuipa nafasi kabisa, lakini hakuna namna tumevuna tulichopanda,” alisema Mogella.
Nyota wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba alisema Simba iliaminishwa na suluhu ya waliyopata ugenini ambayo haikuwa nzuri kwa upande wao.“Ni matokeo ya magumu, lakini hawana budi kukubali, sasa watuunge mkono sisi Yanga tutawabeba kimataifa,” alisema Mziba.
Simba: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gadiel Michael/Mohammed Hussein, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Deo Kanda, Sharaf Shiboub/Miraji Athumani, Meddie Kagere, Clatous Chama na Francis Kahata/Hassani Dilunga.
Katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara zilizochezwa kwenye viwanja viwili tofauti jana, Mwadui ya Shinyanga ilishinda bao 1-0 dhidi ya Singida United wakati Lipuli ya Iringa iliigagadua Mtibwa Sugar ya Morogoro 3-1.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.