BARCELONA, HISPANIA
NAHODHA wa timu ya Barcelona, Lionel Messi, amewatoa wasiwasi mashabiki wa timu hiyo baada ya juzi kuonekana akifanya mazoezi kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu nchini Hispania.
Nyota huyo raia wa nchini Argentina, amekuwa nje ya uwanja kwa siku kadhaa kutokana na kusumbuliwa na tatizo la nyama na kumfanya akose ziara ya timu hiyo nchini Marekani kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi.
Ligi Kuu nchini Hispania inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Ijumaa wiki ijayo ambapo mabingwa wa ligi hiyo Barcelona wakianza kufungua dimba dhidi ya Athletic Bilbao, Barcelona wakiwa ugenini.
Uongozi wa timu ya Barcelona, juzi ulitumia ukurasa wake wa Instagram na kuposti picha mbalimbali zikimuonesha mchezaji huyo akifanya mazoezi ya kujiweka sawa kuelekea ufunguzi wa Ligi wiki ijayo.
Hata hivyo, Barcelona waliweka wazi kuwa, mazoezi hayo aliyaanza kuyafanya tangu Jumatatu wiki hii, hivyo sasa anazidi kuwa vizuri siku hadi siku. Messi mwenyewe alitumia ukurasa wake wa Instagram na kuwatoa wasiwasi mashabiki huku akiwaambia ataonekana uwanjani muda mfupi ujao.
Bado Barcelona ipo nchini Marekani kwa ajili ya maandalizi ya msimu, hivyo watacheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Napoli pamoja na Michigan kabla ya kurudi nchini Hispania.
Hata hivyo, kukosa kwa Messi kwenye michezo hiyo miwili kutaifanya klabu hiyo kukosa kiasi cha pauni milioni 4.5 ambazo zilisainia na baadhi za kampuni kwa ajili ya mchezaji huyo aweze kucheza mbele ya mashabiki zake, lakini kukosekana kwake fedha hizo hazitowekwa mezani.
Mbali na Messi kuonekana akifanya mazoezi, lakini uongozi wa timu hiyo umeweka wazi kuwa, mchezaji huyo anaweza kuukosa mchezo wa kwanza wa ufunguzi dhidi ya Athletic Bilbao ugenini, lakini akaja kuwa kwenye kikosi katika mchezo wao wa pili watakapokuwa kwenye uwanja wa nyumbani dhidi ya Real Betis, Agosti 25.
Post a Comment