KLABU ya Yanga imeingia sokoni na kuongeza nguvu katika maeneo kadhaa katika kikosi chao, lakini eneo la ushambuliaji limekosa mchezaji wa kueleweka, hiyo ni kwa mujibu wa kocha wake wa zamani, Hans van der Pluijm.

Kocha huyo raia wa Uholanzi alisema amefuatilia kwa ukaribu usajili wa wachezaji wapya wa timu yake hiyo ya zamani na kubaini kwamba haina mshambuliaji mwenye kiwango cha kutisha.

Akizungumza na BINGWA jana kutoka Accra nchini Ghana, Pluijm alisema pamoja na klabu hiyo kuwasajili wachezaji wapya akiwamo David Molinga, lakini hana uwezo mkubwa.

Pluijim alisema Yanga inahitaji mpachika mabao wa kuwapatia matokeo bora msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano mingine.

Aliongeza kwamba bado safu ya ushambuliaji ya Yanga ina tatizo kutokana na usajili wao kutofanyika kwa umakini kama ilivyo kwa timu nyingine, ikiwamo Simba na Azam.

Alisema kama Yanga inahitaji kupata matokeo mazuri  msimu ujao ni lazima kocha wa timu hiyo, Mwinyi Zahera ashughulike na safu ya ushambuliaji  kwa kuwa bado haijakaa sawa.

Kocha huyo aliyekuwa na mafanikio makubwa ndani ya Yanga, alisema kutokana na uzoefu wake wa kufundisha soka kwa muda mrefu, hata akiangalia mchezo mmoja wanaweza kubaini mapungufu ya wachezaji.

“Sijaona ule mwamko ndani ya Yanga kama ilivyokuwa  msimu iliyopita labda ligi  bado haijaanza, lakini nazifuatilia sana hizi timu hata mechi zao za kirafiki.

“Kama klabu inahitaji kushinda mechi zake lazima kocha apambane kuwapa mazoezi washambuliaji wake, lakini kwa upande wangu naona bado hata ule umakini wao wakiwa uwanjani haupo sawa,” alisema Pluijm.

Aidha, kocha huyo mzoefu wa soka la Afrika, alisema kwa upande wa mabeki Yanga imefanikiwa kufanya usajili mzuri wa Lamine Moro raia wa Ghana na kiungo mshambuliaji Mnyarwanda, Patrick Sibomana kuwa ameonyesha ari ya kupambana ndani ya kikosi hicho.

Kocha huyo, alisema wachezaji wengine kama Mganda, Juma Balinya na Molinga, wanahitaji muda wa kujifua zaidi ili waweze kufanya vizuri, lakini ikishindikana klabu hiyo ifanye  usajili mwingine katika dirisha dogo.

Pluijm alisema mchezaji mzuri anaweza kucheza katika mazingira ya aina yoyote bila kujali hali ya hewa au uwanja mbovu.

Yanga kwa sasa inakabiliwa na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakitarajiwa kushuka dimbani kesho kuivaa Township Rollers, jijini Gaborone, Botswana baada ya mchezo wa awali kulazimishwa sare ya 1-1, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.