MCHEZO wa soka ni kama kuogelea au kuendesha baiskeli ukijua unajua tu, ndivyo ilivyo kwa kiungo mpya wa Simba kutoka nchini Sudan Kusini, Sharaf Eldin Shiboubo. Ukweli amewiva kila idara uwanjani.

DIMBA Jumatano, ilianza kumfuatilia kwa karibu tangu mchezo wake wa kwanza katika ardhi ya Tanzania aliyoichezea timu yake dhidi ya Power Dynamos ya Zambia katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki kuadhimisha kilele cha tamasha la Simba Day.

Mchezo huo ulipigwa Agosti 6 mwaka huu Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo Shiboubo alionyesha uwezo mkubwa sehemu ya kiungo akiunganisha timu vizuri na pia kusukuma mbele mashambulizi.

Nyota yake iliwaka tena katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC ambapo Msudan huyo alipachiika mabao mawili na kuchagiza ushindi mnono wa mabao 4-2 iliyopata timu yake.

Yote tisa, lakini kikubwa kuliko ni hayo mavitu aliyokuwa akiyafanya katika siku mbili za mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam, ambapo Shiboubo ameonyesha uwezo wa hali ya juu kama wanavyofanya wachezaji mastaa wa timu za ligi maarufu Ulaya.

Katika mazoezi hayo, Shiboubo ameonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kucheza maeneo matatu muhimu; ulinzi, kiungo na hata straika hususan kutokana na kuwa na nguvu na uwezo wa kumiliki mipira.

Kocha mkuu wa Simba, Patrick Aussems, aliliambia DIMBA Jumatano baada ya mazoezi hayo kuwa kikosi chake kinampa matumaini sana, hususan kutokana na ushirikiano wanaoonyesha maeneo mengi ya uwanja.

“Kuna makosa madogo yanaonekana na ndiyo sababu ya mazoezi ili niyabaini na kuyatafutia ufumbuzi,” alisema. Kwa upande wake Shiboubo, alisema anafurahi kuona anafanya kile alichokifuata katika ardhi ya Tanzania, pia anawashukuru mashabiki kwa kujali ambacho timu yao inakifanya

Tags: ,

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.