CATALUNYA, HISPANIA. ILE ‘muvi’ ya Neymar inaendelea na ripoti zinasema straika huyo sasa anakaribia kurejea Barcelona baada ya miamba hao wa Catalunya kupiga hatua kubwa katika mazungumzo na klabu ya PSG.
Mbrazil huyo amedhamiria kurejea Barcelona katika dirisha hili la uhamisho na ameiambia PSG kwamba hatachezea tena klabu hiyo.
Mazungumzo baina ya klabu hizo mbili yalionekana kukwama mapema katika dirisha hili la uhamisho, lakini PSG sasa wako tayari kumuuza Neymar baada ya uhusiano baina ya mchezaji huyo na maofisa wa klabu hiyo kuzidi kuvurugika.
Ripoti zinadai kuwa PSG na Barcelona wamepiga hatua kubwa katika mazungumzo yao hivi sasa kuhusu uhamisho wa mkopo ambao utamwezesha Neymar kusajiliwa jumla katika dirisha la mwisho wa msimu ujao.
Imeripotiwa kuwa Barcelona wamezidi kujiamini kufikia maafikiano na magingwa hao wa Ufaransa.
Uamuzi mzito unatarajiwa kuchukuliwa na PSG wiki hii huku dirisha la usajili (la mataifa mengineyo ukiacha England) likielekea kufungwa Septemba 2. 
PSG hawakutaka kumuuza Neymar katika dirisha hili la uhamisho, lakini wamelazimika kufikiria kumruhusu aondoke kutokana na matendo yake yaliyowafika kooni.
Ripoti zilizopatikana wikiendi zimesema nyota huyo, 27, amewanunia viongozi wa klabu na amegoma hata kuzungumza na Mkurugenzi wa Michezo, Mbrazil mwenzake Leonardo, baada ya kujaribu kuzuia uhamisho wake wa Barcelona.
PSG walishinda mechi yao ya Ngao ya Jamii nchini China juzi Jumamosi bila ya Neymar shukrani kwa mabao ya Kylian Mbappe na Angel Di Maria.
Na wakati wa upigaji wa picha ya timu wakiwa na kombe baada ya mechi uwanjani, Neymar aliposogea ili kupigwa picha, Mbappe alimsukuma kumtoa. Hata hivyo haijajulikana jambo hilo lilikuwa ni ‘siriaz’ kiasi gani kwani Mbappe alikaririwa mwishoni mwa wiki iliyopita akisema kwamba Neymar ni rafiki yake na amemuomba asiondoke PSG.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.