NA ABDULAH MKEYENGE
SIKU chache kutoka sasa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Tanzania utapokea wageni kutoka Zambia.Moja ya wageni hao atakuwa Thaban Kamosoko.
Huyu ni nyota wa zamani wa Yanga na kiungo mpya wa Zesco United. Aliwahi kusema mwanafalsafa mmoja kuwa usimkatie tamaa mwanadamu mpaka awe amelala katika shimo la futi sita.
Kamusoko atakuja na timu ya Zesco United kucheza na Yanga. Wale mashabiki waliowahi kusimama nyuma yake kwa kumpigia makofi, wataenda kugeuka kuwa ‘maadui’. Watamzomea, watamdhihaki. Maisha yamekwenda kasi kwa Kamusoko na Yanga.
Katika mechi ya namna hii ulitarajia kumuona Kamusoko akiwa kiungo wa Yanga, lakini kimaajabu kabisa Kamusoko atakuwa kiungo wa upinzani.Kamusoko si mgeni machoni wala masikioni mwetu. Anakuja katika ardhi ambayo aliwahi kufurahia maisha yake ya mpira. Ni katika ardhi hii alikopata jina na sifa.
Kinachouma zaidi ni kwamba Kamusoko alikuja Yanga siku za mwisho mwisho za Yusuph Manji. Alichokitoa hakikuendena na alichokuwa anakipata.Licha ya kutoa kitu kikubwa na kupata kitu kidogo, lakini alibaki kuwa mchezaji muaminifu.
Alipambana hadi tone lake la mwisho la jasho lake. Hakujali timu inapitia nyakati gani. Alichojali ni kutimiza majukumu yake.
Alitimiza majukumu yake kama mchezaji. Hata alipoondoka watu wa Yanga walimshukuru kwa moyo mmoja. Sijui jinsi watakavyompokea, lakini sidhani kama watamuona kama adui yao.
Kamusoko anaingia katika kundi la wachezaji wa upande mmoja kukubaliwa na mashabiki wa upande mwingine. Wachezaji wa namna hii hawako wengi.
Said Ndemla wa Simba na Abubakar Salum ‘Sure Boy’ wa Azam FC ni miongoni mwao. Ndemla, Sure Boy ni wachezaji wa Simba, Azam FC lakini aghalabu kukuta mashabiki wa Yanga wanawasema vibaya. Kamusoko ni mchezaji wa kariba hii.
Aina yake ya mchezo kiwanjani inamvutia kila mshabiki. Narudia tena wachezaji wa aina hii hawako wengi. Wako wachache wanaohesabika.
Sijui mapokezi yake yatakavyokuwa. Sijui. Lakini sioni kama anaweza kukutana na wakati mgumu. Akizomewa na mashabiki wa Yanga, atashangiliwa na mashabiki wa Simba. Hawezi kukosa vyote.
Sikumbuki njia ambayo Yanga waliitumia kumuaga Kamusoko. Sikumbuki, lakini wanaweza kuutumia mchezo huu kuagana nae vyema. Huyu akamkumbatia yule kumtakia kila la kheri na yule akamkumbatia huyu. Waungwana huwa wanaagana hivi. Kamusoko si mchezaji wa kuagwa juu juu kama vile unamuaga Adam Salamba au Said Makapu.
Muda huu mchache uliobaki kabla ya Kamusoko kuja tena nchini akiwa na jezi za Zesco United tujiandae kumpokea na maua yetu mkononi.
Tumlaki. Tumpeti peti, mwisho kabisa tuwatakie kheri Yanga katika mchezo huo. Kumkumbatia haina maana ndiyo tunataka timu yake iitoe Yanga. Kama Watanzania tusimame pamoja kuitakia kheri Yanga.
@@@@@@@@@@@@@.
Mna bahati nyie, nusu Manara aweke rekodi
ABDULAH MKEYENGE
IMEFICHUKA bwana! Unaambiwa katika Simba Day, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba Hajji Manara alitaka kushuka Uwanja Taifa kutambulisha wachezaji wa Simba kwa usafiri wa Helkopta.
Kuna baadhi ya mambo yalikosekana kidogo tu, lakini mpango mzima ulikuwa umeshasukwa na ilibaki kidogo tu Manara ashuke uwanjani hapo na usafiri huo.
Baada ya mpango huo kushindikana Manara aliamua kuja kivingine kwa kuingia na kundi la Mabaunsa waliomzunguka kila alipokwenda.
@@@@@@@@@@@@.
Post a Comment