BAADA ya kuwaumiza mashabiki wao kutokana na matokeo mabaya ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kikosi cha Simba kimejipanga kuwafuta machozi mashabiki wao kwa kufanya kweli Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba ambao msimu uliopita walifika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, kipindi hiki wameishia hatua ya awali baada ya kutolewa na UD Songo ya Msumbiji. Wekundu wa Msimbazi hao, walianza michuano hiyo kwa sare ya kutofungana nchini Msumbiji, kisha kulazimishwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Kitendo hicho kiliwaumiza wapenzi wengi wa Simba waliohudhuria mechi hiyo kwasababu kila mmoja alikuwa amejiandaa kushangilia ushindi.

Tangu Jumapili iliyopita mchezo huo ulipochezwa, bado hali haijawa nzuri kwa wapenzi wa Simba, hususan kutokana na kejeli zinazoendelea kutoka kwa watani zao Yanga.

Hata hivyo benchi la ufundi la Simba, limekuja na mkakati mpya wa kuhakikisha wanarudisha tabasamu kwa mashabiki wao, mojawapo ikiwa ni kushinda mechi za Ligi Kuu Bara mfululizo.

Malengo yaliyokuwepo si kushinda pekee na kupata pointi tatu, bali ushindi wa mabao mengi kuanzia matano na kuendelea. Kikosi hicho hakijapumzika tangu mchezo wake na UD Songo, kocha mkuu, Patrick Aussems, ameendelea kuumiza kichwa ya kusaka mbinu ya kurejesha furaha Msimbazi.

Tofauti na kocha, benchi zima la ufundi limeungana kuhakikisha kila mmoja anasimama katika nafasi yake kuwaweka sawa wachezaji. Unapofika katika mazoezi yao yanayofanyika viwanja vya Gymkhana, hakuna mtu anayekaa chini, kuanzia meneja, daktari na makocha wasaidizi.

Kila mmoja anahakikisha mchezaji yuko sawa na anafuata programu ya mwalimu kama inavyotakiwa. Akizungumzia mikakati yake, Aussems alisema hakuna kitu kingine anachofikiria kwasasa zaidi ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam litakapoanza.

Alisema hayakuwa matarajio yao kufanya vibaya katika Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini imetokea kutokana na hali ya kimpira na kuwafanya wawe na huzuni msimu huu.

“Malengo yetu kwa sasa ni kufanya vizuri kwenye mashindano yote kuanzia Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na mingine ambayo tutashiriki,” alisema Aussems.

Naye Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema  kitu pekee kitachorudisha furaha kwa haraka ni kushinda mabao kuanzia matato kwenda mbele katika ligi.

“Kuondolewa kwetu mapema kumewaumiza Wanasimba, hata upande wetu kuna vitu tutavikosa, lakini hiki ni kipindi cha mpito tu,” alisema. Simba inatarajia kuanza ligi kesho kwa kuvaana JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Uhuru.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.