ZAINAB IDDY

YANGA imetamba kufika mbali katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wakisema hilo linawezekana kutokana na faida waliyoipata kutokana na ratiba ya michuano ya Kombe la Dunia 2020.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa, Tanzania itavaana na Burundi Septemba 4, mwaka huu kuwania kufuzu fainali hizo za Kombe la Dunia.

Kutokana na hilo, Ligi Kuu Bara itasimama kwa wiki mbili kupisha maandalizi ya timu ya Taifa, Taifa Stars kuelekea mchezo huo dhidi ya Burundi.

Hizo zimekuwa habari njema kwa Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera aliyepania kutumia kipindi hicho kukisuka zaidi kikosi chake, zaidi ikiwa ni kujenga muunganiko wa timu, lakini pia kuwapa wachezaji wake mbinu na ‘maufundi’ yake ili waweze kuwa moto zaidi.

Ikumbukwe kuwa kati ya sababu zilizokifanya kikosi kipya cha Yanga kuonekana kama si lolote, ni kitendo cha Zahera kuchelewa kurejea nchini kuwaunganisha wachezaji wake walipokuwa kambini Morogoro wakati wa maandalizi ya msimu.

Akifahamu hilo, Zahera amejikuta ‘meno nje’ baada ya timu yake kutinga raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, akiamini itakuwa moto zaidi iwapo atakitumia kipindi hiki cha maandalizi ya mechi za kimataifa za kufuzu Kombe la Dunia, kukisuka zaidi kikosi chake.

Mchezo unaofuatia wa Yanga wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga itakutana na Zesco United ya Zambia kati ya Septemba 14 na 15, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni baada ya kuitoa Township Rollers ya Botswana kwa jumla ya bao 1-0.

Lakini kabla ya kukutana na Zesco United, Yanga itakuwa na mchezo wa Ligi Kuu Bara keshokutwa Jumatano dhidi ya Ruvu Shooring kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza na BINGWA kutoka Botswana, Makamu Mwenyenyekiti wa Yanga, Fredick Mwakalebela, alisema kuwa mara baada ya mechi yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting, kikosi chao kitakwenda mafichoni.

“Baada ya mechi za kwanza za Ligi Kuu, ligi itasimama kupisha mechi za timu ya Taifa, kipindi hicho tunahitaji kuweka kambi ya muda na wachezajia mbao hawajaitwa timu za taifa.

“Mara baada ya mechi jana (juzi), tulikaa na wachezaji pomoja na Watanzania walioko Botswana kuwapongeza, kisha viongozi tukakaa faragha na kocha Zahera kujua mikakati yake ijayo.

“Zahera ameomba awe na kambi baada ya mechi dhidi ya Ruvu Shooting, ndipo tulipompa jukumu la kuchagua wapi anataka aende na wachezaji hadi pale mechi yetu na Zesco itakapokaribia, ndipo timu irejee Dar es Salaam.

“Sehemu gani timu itakwenda kujificha, tutajua mara baada ya mechi na Ruvu Shooting, Zesco sio timu ya kuipuuza lazima tuwe na maandalizi mazuri ili tutimize malengo ya kusonga mbele Ligi ya Mabingwa Afrika.”

Yanga ilitaraji kurejea nchini jana jioni ikitokea Botswana na kuingia kambini moja kwa moja kujiandaa na mechi dhidi ya Ruvu Shooting.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.