CATALUNYA, Hispania
HATA msimu uliopita, majeraha yalikuwa chanzo kikubwa cha fowadi wa Barcelona, Ousmane Dembele, kushindwa kutamba. Safari hii, balaa limemrudia na atakuwa nje ya uwanja kwa wiki tano.
Kwa mujibu wa mtandao wa klabu ya Barca, watamkosa nyota wao huyo kuwa ameumia nyama za paja, pigo kubwa kwa kikosi hicho baada ya Luis Suarez na Lionel Messi nao kuumia.
Dembele alionekana akichechemea wakati Barca wakiadhibiwa kwa kichapo cha bao 1-0 na Athletic Bilbao, mchezo wa kwanza kwa kila timu tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’.
Mfaransa huyo, ambaye ni mshindi wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka jana kule Urusi, alitua Barca mwaka juzi akitokea Borussia Dortmund, ada ya usajili wake ikiwa gumzo, Pauni milioni 100 (zaidi ya Sh bil. 270 za Tanzania).
Post a Comment