Juventus iliingilia kati na kuipa United ofa ya Pauni 10 milioni pamoja na mastaa wake wawili, Dybala na Mario Mandzukic lakini ni Dybala ndiye ambaye ameukonga moyo wa Kocha Solskjaer na sasa amekubali kubadilishana naye na Lukaku.

MANCHESTER,ENGLAND.TAYARI mchezo umeisha. Wakubwa wameafikiana kwamba Romelu Lukaku aende Juventus na Paulo Dybala aende Manchester United. Hii ni kiroho safi bila ya ugomvi na anayesubiriwa kwa sasa ni Dybala kukubali dili hilo.

Inafahamika Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer hana mpango tena na Lukaku na alimuacha staa huyo wa kimataifa wa Ubelgiji nyumbani wakati timu iliposafiri kwenda Norway juzi kucheza mechi ya kirafiki na Kristiansund.

Kabla ya hapo Lukaku alionekana kuelekea Inter Milan lakini uhamisho huo umesuasua baada ya mabosi wa Inter kugoma kutoa kiasi cha Pauni 75 milioni ambacho United ilikuwa inakitaka kwa ajili ya kumuuza Lukaku.

Juventus iliingilia kati na kuipa United ofa ya Pauni 10 milioni pamoja na mastaa wake wawili, Dybala na Mario Mandzukic lakini ni Dybala ndiye ambaye ameukonga moyo wa Kocha Solskjaer na sasa amekubali kubadilishana naye na Lukaku.

Na sasa anayesubiriwa ni Dybala tu kukubali dili hilo na kukubaliana maslahi binafsi na Manchester United huku ikielezwa staa huyo ana nafasi kubwa ya kukubali uhamisho huo baada ya nafasi yake ya kucheza kikosini Juve kupungua tangu kutua kwa Cristiano Ronaldo kutoka Real Madrid katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka jana.

Inaeleweka wakala wa Dybala yupo London kwa sasa kwa ajili ya mazungumzo na United na inafahamika staa huyo wa zamani wa Palermo analipwa kiasi cha Pauni 120,000 na Juventus katika mkataba wake wa sasa.

Kwa upande wa Lukaku, staa huyo wa zamani wa Everton na Chelsea amekuwa akichukua kiasi cha Pauni 200,000 kwa wiki tangu atue klabuni hapo miaka miwili iliyopita. United itanufaika kwa kumpa Dybala mshahara wa chini ya dau hilo ambalo inatazamiwa kumpa Pauni 176,000 kwa wiki.

Kocha wa United, Solskjaer alikiri baada ya pambano dhidi ya Kristiansund lililofanyika nyumbani kwao, Norway na United kushinda 1-0 kwamba klabu yake imekuwa ikitafuta sura mpya kabla ya kuanza kwa ligi Agosti 9.

“Sipo hapa kuongelea kuhusu uvumi wa wachezaji wa timu nyingine. Lakini ni kweli kwamba tunafanyia kazi uhamisho wa mchezaji mmoja au wawili kama nilivyosema hapo awali. Kuna siku nyingine kumi kabla ya kuanza kwa ligi na tuna matumaini tutakuwa na sura moja au mbili mpya,” alisema Solskjaer.

Hata hivyo, kocha huyo ambaye ni staa wa zamani wa United alikuwa mjanja kuhusu suala la kumuacha Lukaku nyumbani wakati timu ikienda Norway huku akidai ilitokana na mshambuliaji huyo kuwa majeruhi.

“Alikuwa ameumia. Lilikuwa jambo bora kwake kubakia nyumbani. Asingeweza kucheza. Tuna matumaini ataweza kufanya mazoezi siku chache zijazo. Tusubiri kuona kitakachotokea,” alisema Solskjaer

“Hauwezi kujua kitakachotokea katika soka. Hajaweza kufanya mazoezi, ilibidi tumrudishe nyumbani. Bado tulikuwa na matumaini angeweza kuwa fiti kwa safari za Australia, Shanghai na Singapore. Lakini kwa safari hii fupi hakukuwa na haja ya kumleta.”

Na sasa Solskjaer atakuwa akitazamia Dybala apatikane kabla ya pambano la kwanza la Ligi Kuu ya Egland dhidi ya Chelsea, Agosti 11.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.