Masau Bwire ni miongoni mwa wasemaji wenye maneno ya kebehi kwa timu pinzani katika mechi wanazokutana, maneno ambayo yamempa umaarufu kwa wasemaji wa klabu za soka nchini.
Dar es Salaam.Habari ya mjini hivi sasa ni Ofisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire kuhusishwa kuchukua nafasi ya Dismas Ten ndani Yanga, lakini mwenyewe amevunja ukimya.
Masau ni miongoni mwa maofisa Habari wa klabu za Ligi Kuu nchini wenye umaarufu amesema kama Yanga watamhitaji kipindi hiki haitokuwa mara ya kwanza kufanya hivyo.
"Wamewahi kunifuata japo ni kipindi cha nyuma ili niwe msemaji wao, wakati ule hata Dismas Ten hakuwa Yanga, nilizungumza nao, lakini sikuwa tayari kwa wakati ule," alisema Masau Bwire.
Alisema kutakiwa kipindi hiki ili awe msemaji si kweli kwani Yanga hawajawahi kumfuata zaidi ya yeye pia kusikia taarifa hizo kwenye mitandao ya kijamii.
"Lisemwalo lipo, kama halipo basi linakuja, hivyo nasubiri litakapotokea Yanga kunifuata ndipo nitakuwa katika nafasi nzuri ya kuzungumza hatma yangu," alisema Bwire.
Alipoulizwa sababu za kutojiunga na timu hiyo walipomfuata awali alisema wakati ule hakuweza kuiacha Ruvu Shooting iliyokuwa katika matatizo ya kushuka daraja.
"Nisingeweza kuondoka kipindi kile kwani tafsili yake ingekuwa baada ya kuona imeshuka daraja ndipo naikimbia, jambo ambalo sikutaka lizungumzwe, hivyo Yanga waliponifuata niliwambia bado na majukumu ya Ruvu Shooting," alisema Bwire.
Bwire alisema yeye falsafara yake ni kazi kwanza pesa baadae, hivyo kama Yanga kweli inahitaji huduma yake ya usemaji wa klabu kama inavyozungumzwa itamfuata ili wazungumze lakini kwa sasa hakuna mawasiliano yoyote aliyofanya na uongozi wa klabu hiyo.
Post a Comment