TANGU Machi 17, mwaka huu lilipotoka tamko la Serikali kuzuia mikusanyiko isiyo ya lazima na kusitisha shughuli mbalimbali ikiwemo michezo kutokana na janga la Virusi vya Corona, kuna maoni mbalimbali yamekuwa yakitolewa.


Tamko la Serikali ni ndani ya siku 30 ndiyo marufuku hiyo itatakiwa kufuatwa, lakini pia itaangalia na namna hali ya hewa itakavyokuwa kwa maana ya hivyo virusi vitakuwaje maambukizi yake.

Kusimamishwa kwa michezo kumezifanya ligi zetu kusimama, hii si Tanzana tu, bali ulimwenguni kote kwa sasa. Hapo awali ilikuwa kwa baadhi ya nchi, lakini sasa ni kote.

Bado hatujafahamu siku sahihi ambayo ligi yetu itaendelea, lakini kwa taarifa za awali hizo siku 30 zilizotolewa awali ni sehemu ya kuangalia namna tatizo litakuwaje.

Lakini upande mwingine kuna watu wamekuwa wakitoa maoni kwamba ni bora msimu huu ufutwe, tuanze upya msimu ujao.

Ni mawazo ya mtu au watu fulani ambayo kufuatwa ni uamuzi wa wenye mamlaka, lakini si vibaya kuyachukua mawazo hayo.

Katika namna ya kutoa uamuzi, suala hilo lipo chini ya mamlaka husika kwa maana ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo lina kamati zake zinazosimamia ligi zetu.

Pia kama tatizo hili litaendelea kuwepo siku zaidi ya zile ambazo zimetolewa awali kama angalizo, basi uamuzi wa busara uchukuliwe. Iwe kuufuta msimu au kuamua ligi zimalizike kwa staili gani.

Tusifuate mkumbo wa wenzetu wamefanya nini, kisha sisi tukapita mulemule. Tunapaswa kuwa na kauli yetu kama sisi Watanzania, wala tusiangalie wengine walichofanya.

Nimesikia Ubelgiji hatua ambayo wamefikia ni kuufuta msimu hapo ulipofikia na kumpata bingwa. Kwetu hatujafikia hatua hiyo.

Kama ikifikia hatua hiyo, tuangalie namna itakavyokuwa. Wale waliokuwa wanakaribia kupanda daraja, kuwa mabingwa na kushuka daraja itakuwaje.

Mfano msimu ukifutwa hapa ulipofikia, kisha ikachukuliwa msimamo ulivyo kutafuta mshindi na wa kushuka daraja, zipo timu ambazo zitaumia.

Kwa ligi kuu pekee, Simba inaonekana kuwa karibu kuwa bingwa, Singida United ipo karibu kabisa kushuka daraja.
Ligi Daraja la Kwanza Kundi B, Gwambina imebakiwa na pointi tatu tu ipande daraja, lakini pia kuna timu zipo kwenye hatari ya kushuka daraja.

Kwa mfano wa ligi hizo mbili, ikichukuliwa uamuzi wa ligi kufutwa kisha wahusika wakasema misimamo kama ilivyo ndiyo iamue nani awe bingwa na nani ashuke daraja na kupanda, wapo watakaoumia hasa wale ambao katika mechi zilizobaki walikuwa na uhakika wa kushinda na kujinasua na janga la kushuka daraja.

Lakini wakisema ligi zifutwe, kisha kila ligi msimu wake uanze upya, kuna timu ambazo zimefanya vizuri msimu huu na kubakiwa na asilimia chache kufikia malengo, zikashindwa kutamba tena msimu ujao, hapo zitadhulumiwa.
Mwisho kabisa, wahusika ambao ni TFF ndiyo wenye kauli ya mwisho endapo hali hii ya hatari itaendelea kuwepo hata baada ya muda uliopangwa kupita.

Kikubwa mimi na wewe tuombe hili janga liondoke na mambo yaende kama zamani, sidhani kama hakuna mtu aliyekuwa hajamisi kuona soka likichezwa. Wote tumemisi, basi tuombe Corona iondoke, lakini pia tujikinge kwa kufuata maelekezo ya wataalamu tusiwe waathirika.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.