NA SALEH ALLY
ITAKUWA si vibaya kukumbusha mambo ambayo tunaamini yatakuwa na msaada katika maendeleo ya mpira wetu nchini.
Bila ubishi, kuna mengi tumejadili na huenda hatukuyafanyia kazi lakini leo kuna kitu kinaweza kuwa kinaonekana na kinaonyesha kile tulichokijadili hatukukifanyia kazi bure na tungekifanyia, kingeuokoa mpira wetu.
Mimi ni kati ya watu wanaounga mkono klabu hasa hizi kongwe kwenda katika mabadiliko kwa maana ya uwekezaji, hakuna ubishi. Lakini bado nimekuwa nikisisitiza suala la ubunifu kwa ajili ya kuongeza thamani ya klabu hizo.
Simba leo inataka inunuliwe bilioni 20 kama sehemu ya takriban nusu ya thamani yake. Mimi naweza kusema ingeweza kununuliwa kwa pauni bilioni 50 angalau kwa nusu ya thamani yake.
Bei kuwa chini inatokana na Simba kukosa mambo mengi ambayo yangeifanya kuwa na thamani ya juu na mwekezaji angeona anastahili kuweka fedha nyingi zaidi.
Mwekezaji ni mfanyabiashara, lazima aangalie hesabu zake kama anataka kuingiza fedha. Mbele ya watu anaweza kusema ana mapenzi lakini kwa mfanyabiashara tunajua, rafiki namba moja ni faida, sote tunalielewa hili.
Hakuna mfanyabiashara asiyeangalia faida, hata anachowekeza anaangalia faida na hili halina ubishi. Hivyo thamani inakuwa ndogo kutokana na viongozi waliopita na waliopo sasa kutokuwa wabunifu, ndiyo maana Simba inaweza kubanwa na mtu au kampuni kwa kuwa mashabiki na wanachama nao wanafurahia ushindi wa siku moja, wiki moja au msimu mmoja.
Kwa kifupi Simba na Yanga zimekuwa zikiishi maisha ya msimu mmoja pekee. Hazijui kuna kesho, ndio maana zinabaki palepale na mabadiliko makubwa yakiwa ni usajili wa wachezaji wapya na jezi mpya za msimu. Yaliyobaki, hayana tofauti na ya msimu uliopita.
Umeona katika mgogoro wa siku chache zilizopita kati ya wadhamini ambao waliamua kujitolea kuidhamini Yanga hadi nje ya mkataba.
Mkataba wa Yanga na GSM ni suala la uuzwaji wa jezi. Lakini wao GSM wakawa na mapenzi binafsi ambayo bado ninasema ni mazuri lakini kwa mfanyabiashara yeyote, lazima atakuwa ana mawazo ya kibiashara.
Ndio maana GSM nao inafikia wanatamani kuona wanapata kitu kama wafanyabiashara, kama wametoa chao cha ziada nje ya mkataba si vibaya kupata cha nje ya mkataba.
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga wao wanataka utaratibu ufuatwe lakini ukiangalia nguvu ya kufanya utaratibu ufuatwe haipo kwa kuwa hakuna nguvu ya kifedha kutosha kuwasajili wachezaji.
Mfano Yanga ingekuwa yenyewe tu imewasajili wachezaji kwa fedha zake, GSM wangekuwa hawana uwezo wa kuingia huko. Lakini kwa kuwa wanatoa fedha zao, halafu wanapangiwa kila kitu, itawezekana vipi?
Kuna jambo la kujifunza hapa pia kwamba Yanga ingekuwa na uwezo wa kupata fedha zake yenyewe, kusajili na kufanya mambo yote na wadhamini wangebaki kuwa wadhamini na kupata haki zao kwa mujibu wa mkataba.
Wanaweza kuingia hadi ndani kwa kuwa mwenye nyumba hana nguvu licha ya kuwa anazo nguvu. Kinachomshinda ni yeye kuzipangilia nguvu zake ziwe na uhakika wa kufanya yaliyo sahihi bila ya watu wengine kuingia.
Hili ni somo na tukubali, Yanga au Simba zinakosa hiyo nguvu kwa kuwa mipango yao imekuwa ni kuishi leo tu na kujali zaidi furaha ya leo bila ya kuangalia maisha ya kesho yatakuwaje.
Yanga na Simba wanaamini maisha ni leo tu, wanaona kama kesho hawatakuwepo au haiwahusu na hili ni tatizo kubwa linalowaangusha na itaendelea kuwa hivi kwa kuwa viongozi wanaishi maisha ya leo pekee.
Lazima kubadilika, lazima kujitathmini na kama mnataka nguvu ya utaratibu, basi kuweni wabunifu kuzifanya klabu zenu imara kifedha ili zijitegemee na kuwa na maamuzi yake la sivyo, mtakuwa mkilalamika sana kila kukicha bila ya jibu sahihi.
Post a Comment