NAJUA nimekuwa gumzo kubwa kutokana na maendeleo ambayo nimekuwa nikianza kuyapata taratibu katika mchezo wa soka, ndio maana hata ukiwauliza wapenda mpira majina matatu au manne ya makipa wazuri, leo wanaweza kusema mmoja wao ni Metacha Mnata.


Hadi kufikia hapa, nimepita sehemu nyingi sana ambazo inawezekana kuna ugumu kidogo watu kujua na inawezekana wakaona ilitokea tu nikawa Yanga kibahati, la hasha.

Nimepambana sana na kupita katika sehemu nyingi sana. Nimekutana na changamoto za kila aina lakini nimekuwa ni mtu ambaye nilitaka kufikia sehemu fulani na ningependa kwenda zaidi ya hapa kwa kuwa mimi si mtu mwepesi kukata tamaa.


Pamoja na kuwa Yanga, sasa mimi ni kipa wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars na naendelea kuwa kati ya makipa wanaochipukia kwa kasi lakini najua walio chini yangu wako wengi bora sana, walio juu yangu, wako wengi bora sana, hivyo nimekuwa nikiendelea kujituma kuhakikisha nafikia ndoto zangu.


Nilijiunga na Yanga baada ya Azam FC kukubali kwa kuwa wao ndio walikuwa wananimiliki na walikuwa wamenipeleka Mbao FC kuendelea kujiweka sawa kwa maana ya kupata nafasi ya kucheza katika kikosi chao kulikuwa na ugumu maana wao tayari walikuwa na makipa wengi.


Aishi Manula, Mwadini Ally ni kati ya makipa waliochangia mimi kupelekwa kwa mkopo Mbao FC na hii ilikuwa ni kutokana na mimi kuonekana ndio nilikuwa nachipukia.


Katika hali ya kawaida, lazima mtu ungejikuta unakata tamaa lakini kwangu nilichukulia kama sehemu ya changamoto ya maisha na sehemu ya kukua kisoka kwa vile hakuwezi kuwa na safari iliyonyooka tu bila ya kupitia katika milima na mabonde.



Ndio maana unaniona leo hapa baada ya kuwa tumesimamishwa kuendelea na kazi kutokana na janga la ugonjwa wa Corona, mimi bado naendelea kujifua. Naendelea kupambana na kujiweka fiti kwa kuwa najua natakiwa kuwa na utimamu wa mwili na kwa makipa ukibweteka kidogo tu basi uzito unapanda kwa kasi na inakuwa kazi kurejea katika kiwango chako.


Kawaida nimekuwa nikiendelea na mazoezi kwenye ufukwe mmoja wa Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha nakuwa fiti nikishirikiana na mwenzangu. Lengo ni kuwa fiti hata kama itatokea ligi imeanza ndani ya muda mfupi au ikatokea tumeanza kucheza na Yanga inanihitaji hata kwa mechi ya kirafiki.



SAFARI:
Safari yangu ya maisha kisoka haikuwa rahisi kama ambavyo nilisema awali. Najua hata wakati fulani watu waliwahi kuhoji kuhusiana na jina langu, wakijiuliza kama kweli ni Mtanzania lakini ukweli hasa mimi ni Mtanzania kamili na nimezaliwa na kukulia mkoani Dodoma ingawa kwetu kiasili ni kule Musoma.


Dodoma ndipo nilianza kukua kisoka, kuna timu inaitwa Panama ndio ilinilea kisoka. Niliendelea kupambana pale hadi siku moja niliposhauriwa niende nikatafute timu na kucheza michuano ya Under 20, hii ilikuwa ni baada ya kumaliza shule. Nikafanya hivyo na niliona Dar es Salaam ni sehemu sahihi, nikafunga safari kuja huku na nilipofika tu nikafikia kwa dada yangu.


 Hapa Dar es Salaam wakati wa pilika za kutafuta sehemu sahihi nikakutana na kipa wa zamani wa Simba, Spear Mbwembwe. Nilimueleza nilichokuwa nikihitaji, akanichukua na kuanza kuwa ananipa mazoezi na mafunzo kuhakikisha nakuwa katika kiwango cha ushindani.


Niliendelea kufanya hivyo hadi ikafikia siku yeye aliona kwamba sasa nimekuwa fiti. Akaniambia wewe uko tayari na unaweza kwenda kutafuta timu. Lakini baadaye akaniahidi kwamba angenitafutia timu ya under 20 ili nijiendeleze. Akasema atafanya hivyo na mimi ataniachia kazi ya kupambana huko kupata nafasi kutokana na juhudi zangu.


Baada ya siku chache alinipigia simu na kuniambia kesho yake nilitakiwa kutoka Gongo la Mboto saa 10 usiku ili niende Chamazi katika kambi ya Azam FC. Basi nilimsikiliza, na mimi muda ule nikaondoka kwenda Chamazi, siku iliyofuata hiyo. Lakini bahati mbaya mimi  nilichelewa, kumbe siku hiyo ulikuwa unafanyika usaili chini ya yule kocha mmoja raia wa India anaitwa Vivic.


Nikajipenyeza wakati walinzi wanafunga geti, tayari watu walikuwa wamechaguliwa na hatua ilikuwa imefika ya mwisho na kama ukishinda pale unapewa nafasi ya kuwa unafanya mazoezi na U20 ya Azam FC lakini unakuwa hauingii kambini. Badala yake unakuwa unakwenda nyumbani na kurudi.


 Yule kocha aliponiona huenda kutokana na kuwa na mwonekano wa ukipa hivi na nilivyokuwa nimevaa, akavutiwa na mimi na kunipa nafasi, nikacheza vizuri nikadaka na penalti na akaniambia niendelee kuja, nikawa nafanya hivyo.


Baada ya hapo nikaruhusiwa kuwa kati ya wale watu wanaotakiwa kuendelea na mazoezi. Lakini yule Kocha Mhindi hakutaka tuendelee kukaa pale lakini kocha wa makipa akawa anatuficha mabwenini, anakwenda anatuletea chakula tunakula tukiwa tumejificha na ukifika wakati wa mazoezi tunaibuka na kuungana na wenzetu.


Baada ya muda mfupi, ajabu yule kocha Mhindi tena akaamua kwamba tuondoke. Akatufukuza mimi na baadhi ya wenzangu.


ILIKUWAJE Metacha akatimuliwa na Kocha Mhindi ambaye alitaka apewe nafasi ya kufanya mazoezi? ENDELEA KUFUATILIA KESHO.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.