UPO uwezekano mkubwa wa mastaa wakubwa Simba kutimka kwenye klabu hiyo kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu Bara baada ya kupata ofa nono za kucheza soka nje ya nchi, ikiwemo Afrika Kusini.

Mastaa hao wanaotaka kuondoka Simba wote mikataba yao inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu ambao ni Sharraf Eldin Shiboub na Hassani Dilunga huku mmoja Clatous Chama akiwa na mkataba wa mwaka mmoja.

Kati ya wachezaji hao, wapo wale ambao tayari uongozi wa Simba umeanza mazungumzo nao kwa ajili ya kuwaongezea mikataba ya kuendelea kukipiga Simba kwenye msimu ujao.

Habari zinaeleza Chama anahitajika na moja na klabu kubwa Afrika Kusini ambayo ipo kwenye mazungumzo huku Yanga ikitajwa nayo kuwania saini yake.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa Dilunga anahitajika na nchi za Afrika Kusini na Uarabuni na huenda akatimka mara baada ya maambukizi ya Virusi vya Corona kumalizika.

Aliongeza kuwa na Shiboub anahitajika na klabu kubwa za Afrika Kusini, Sudan na Misri ambazo zote zimeonyesha nia ya kumhitaji na yeye mwenyewe ameomba aondoke kwa kile kinachodaiwa kutokuwa na mahusiano mazuri na kocha mpya, Mbelgiji Sven Vandenbroeck.

“Simba huenda ikapata pigo kubwa la kuondokewa na viungo wake watatu wakubwa katika msimu ujao wa ligi, ni baada ya wachezaji wenyewe kuonekana kutaka kuondoka.

“Kati ya wachezaji hao wanaotaka kuondoka, wawili wameonekana kutokuwa na furaha na timu hiyo kwa kile kilichoelezwa kutokuwa na mahusiano mazuri na kocha.

“Wachezaji hao walifuatwa na viongozi kwa ajili ya kuongeza mikataba mipya lakini wameomba mazungumzo yafanyike mara baada ya mikataba yao kumalizika,” alisema mtoa taarifa huyo.
  
Aidha, Ofisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Senzo Mazingisa hivi karibuni alisema kuwa timu yao haitakubali kumuachia mchezaji yeyote watakayemuhitaji ambaye mkataba wake unamalizika na badala yake itapambana kumbakisha.

Chanzo: Championi

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.