NIMESIKIA kuna mpango wa kuzitaka timu za ligi kuu kuwa na timu za vijana chini ya miaka 15.
Ni wazo zuri ambalo litasaidia sana kuzalisha wachezaji ambao watakuwa faida kubwa kwa siku za baadae.

Wenzetu wote walioendelea waliwekeza kwenye soka la vijana na leo hii wanaringa na mafanikio yao.
Wenzetu walianza kitambo sana na walijua nini faida ndio maana leo wanakula matunda yake tena kwa raha kubwa.

Sisi kama tutakuwa makini na mpango huo nina hakika tutafanikiwa tena sio siku nyingi ndani ya miaka mitano tu au mbele kidogo.

Tatizo langu ni kwamba je tutaweza kulisimamia suala hilo ambalo ni kubwa mno sio la mchezomchezo.

Nasema hivyo kutokana na jinsi historia ilivyo kwenye soka letu ambalo tunaanzisha mambo mengi ila kuyaendeleza ni tatizo.

Nakumbuka kuna kanuni ya ligi kuu inayoziamuru timu zote za ligi kuu kuwa na timu za vijana za chini ya miaka 20, lakini utekelezaji wake wote tunaujua.

Timu nyingi za ligi kuu hazina timu imara za hao vijana na hata hao TFF wanajua sasa wanakuja na huo mpango wa chini ya miaka 15.

Kikubwa ni kwamba timu zetu nyingi za ligi kuu hadi daraja la kwanza zina hali mbaya kiuchumi na haziwezi kuziendesha hizo timu za vijana chini ya miaka 20, sasa zitaweza kuendesha timu za miaka 15?

Hapa kuna matatizo mawili ya kiuchumi na uelewa hasa kwa hao viongozi wa timu ambao sijui kama watalipokea kwa umakini unaotakiwa.

Nilipomsikia Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Oscar Mirambo analielezea suala hilo nilijawa na maswali mengi lakini acha niseme kweli nimelipenda wazo lake na lina faida kwa soka la nchi hii, lakini tatizo ni mfumo wetu.

Uwekezaji ni mdogo mno kwenye soka letu ambalo hadi leo hatujui thamani halisi ya ligi yetu na wengi wanashindwa kulijibu swali hilo kwa sababu wanajua mateso yanayotokea kwenye klabu.

Wenzetu soka ni biashara kubwa tena yenye kuingiza mamilioni ya fedha ndio maana wanafanya wanavyotaka ila kwetu ni tatizo kwa sababu timu zetu ni maskini na hazina pesa kabisa.

Klabu nyingi za Bongo zinalia njaa, hali ni ngumu kwao na sasa hao watu wanapewa mzigo wa timu za chini ya miaka 15 sijui kama wataweza kuubeba.

Sidhani kama ulifanyika uchunguzi wa namna klabu zetu zilivyo, kisha ndiyo kuja na suala hilo la kuwa na timu za chini ya miaka 15.

Kama nilivyoeleza hapo awali, hivi sasa timu za ligi kuu zina timu za vijana chini ya miaka 20, zamani kulikuwa na mpango wa kila timu ikienda kucheza mechi ya ligi, basi zitaanza kupambana timu zao za vijana, ndipo wakubwa wanafuata.

Lakini mara kadhaa tumeshuhudia pale Uwanja wa Taifa jijini Dar, Simba ikiwa inacheza na Mbao, basi vijana wa Simba wanatafutiwa timu yoyote kucheza nayo, kisha ndiyo wakubwa wanafuata, na wakati mwingine hakuna kabisa hizo mechi za vijana.

Kinachopendeza ni kwamba, siku ya mechi ya watani, Simba dhidi ya Yanga, ndiyo huwa tunashuhudia mengi, vijana wao wanaanza kukipiga, kisha wakubwa wanafuata.

Sasa huu mpango wa sasa wa kuwa na timu za vijana chini ya miaka 15 ulifanyiwa uchunguzi kabla au kupeana mizigo tu.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.