JUZI Jumatatu nilielezea namna ambavyo nilishindwa kuendelea kucheza na kidole kilichovunjika na kulazimika kusema na matibabu yakaanza kupitia yule mama ambaye hakuwa akitumia tiba kama za hospitali.
Kama unakumbuka nilieleza nilivyoamua pia kuondoka Prisons na kurudi tena Mbao FC kwa kuwa sikuona kama kungekuwa na maisha ya mbele yenye mwendelezo pake Mbeya. Ilikuwa shida na ilionekana kama hawataki kuniachia.
Baada ya msisitizo wangu kuwa mkubwa, wakasema kuna fedha walitoa wakati wakinichukua kwa mkopo kutoka Azam FC, mwisho nikawaambia nitarudisha ili niondoke. Siku chache baadaye nilizungumza na watu wa Mbao FC ambao walikubali kulipa fedha ile kwa Prisons kwa kuwa kweli walikuwa wakivutiwa na kazi yangu.
Mbao FC wakafanya vile baada ya Prisons kunipa barua kuwa tumemalizana na mwisho ikawa rasmi kweli na mimi nimerudi Mbao FC kwa mara nyingine tena.
Nilimkuta Amri Said, nikafanya naye mazoezi kama wiki tu akaondoka. Akaja kipa Ali Bushiri ambaye aliwahi kuwa kipa, akawa anatusaidia sana katika mazoezi.
Kiwango changu taratibu kiliimarika ingawa mechi mbili za mwanzo tulitolewa na Dar City, mechimbili zilizofuata za Ligi Kuu Bara tukashinda na tayari nikawa nimerudi ndani ya Mbao FC kwa maana ya kutulia tena.
Siku chache baadaye tukaingia katika michuano ya SportPesa Super Cup na kama unakumbuka tulikutana na Simba mshindi wa tatu. Baada ya mashindano hayo nikatangazwa kuwa kipa bora wa michuano hiyo, lilikuwa jambo la faraja sana kwangu.
Baada ya mashindano hayo ndio nikaanza kupata simu kutoka kwa watu wa Yanga wakiniambia walikuwa wanataka nijiunge nao. Nikawaambia wawasiliane na mtu ambaye anasimamia, wakaanza kuwasiliana.
Siku chache baadaye nikaitwa timu kubwa ya taifa, sikupata nafasi ya kucheza lakini nikaendelea vizuri hadi nikapata nafasi ya kwenda Misri kwenye Afcon. Nikiwa kule, Yanga wakamalizana na meneja na mwisho wakaja kule Cairo na nikasaini mkataba nao.
Wakati huo nguvu ilikuwa Afcon na kama unakumbuka nilipata nafasi ya kucheza mechi ya mwisho dhidi ya Algeria, ingawa tulipoteza lakini nilijitahidi sana.
Mwanzo nilianza na hofu kubwa, unajua mashindano yale ni makubwa sana. Kipindi cha kwanza kilikuwa kigumu lakini mapumziko kocha akanipa moyo na niliporejea nikajitahidi.
Ushindani ni mkubwa kila sehemu, mfano hata hapa Yanga kuna ushindani wa juu kabisa. Farouk (Shikalo) ni kipa mkubwa, ana vitu vingi kunizidi mimi na ninakubali kabisa. Naendelea kujifunza kupitia kwake hata kama tunapata wote nafasi ya kucheza lakini yeye ana vitu vya ziada, ukimuona golini lazima utatamani vitu fulani alivyonavyo uwe navyo.
Kabwili pia ni mzuri, hata kama hajadaka lakini unaona mazoezini ni kipa mzuri kabisa. Tunaendelea kuhamasishana kwa ubora na tunafanya kazi yetu vizuri.
Kingine ni kuhusiana na ushindani katika ligi na unaona mechi za Yanga ni tofauti sana maana kunakuwa na presha kubwa sana. Mbao unaweza kufungwa kwa makosa yako ukarekebisha lakini Yanga hata ukifungwa bao la mchezoni utasikia mashabiki wanasema ni bao rahisi. Wakakupa presha kubwa sana ingawa kwangu mimi naona hiyo ina uzuri wake wakati mwingine maana inakuongezea kufanya juhudi zaidi.
Binafsi napenda nikicheza niisaidie timu, mfano mechi ya Simba na Yanga ilikuwa na presha sana. Kitu kizuri katika ile mechi kocha aliniambia mapema kabisa kuwa nitacheza baada ya kucheza mechi mbili.
Akaniambia nakupumzisha usije ukapata kadi, unajua baada ya mechi na Alliance nikawa na kadi mbili za njano. Kocha akaniambia ananipumzisha na akanisisitiza niendelee kufanya mazoezi kwa jitihada, nami nikaanza kujiandaa mapema maana naijua mechi. Hivyo nilikuwa tayari kabisa ingawa kidogo mwanzoni nilikuwa nna hofu lakini baada ya muda nikatulia.
Makocha wote, Luc Eymael, baadaye Manyika Peter na Kocha Mkwasa pia naye akaja wakanieleza kuwa mechi hiyo ni ngumu nje ya uwanja lakini ndani ni mechi nyepesi sana na ninaiweza.
Nashukuru nilifanya vizuri ingawa ile double save nilifanya, shuti la kwanza la yule Luis Miquissone alipiga katika kipindi ambacho hautegemei, nikaokoa. Akaja Chama naye akapiga, lakini nikafanikiwa kuokoa kwa mara nyingine. Sijasahau hadi leo.
Kingine kigumu katika mechi ile ilikuwa ni dhidi ya Kagere. Alipiga lile shuti lililogonga mwamba ambalo kwa namna ambavyo nilikuwa natarajia ilikuwa ni vigumu sana kuokoa. Nimpongeze kwa kile alichokifanya lakini ni kati ya mambo ninayoendelea kujifunza.
Kuhusiana na kuoa watu walipata hofu, kwamba nimesajiliwa tu baada ya muda nikaoa. Uhalisia ni kwamba mimi nilishakuwa nimekaa naye muda mrefu, hivyo nilikwenda kubariki. Mke wangu tumepambana mambo na changamoto nyingi na nikiri amenisaidia sana na kumuoa ilikuwa ni kuzidi kuomba baraka za Mungu azidi kufungua njia kwa kuwa nilifanya jambo la baraka.
Mwisho nataka kucheza nje na kama mambo yakiwezekana, kokote nitakapopata timu na ndio maana naendelea sana kujituma.
Post a Comment