NAHODHA wa timu ya Coastal Union, Bakari Mwamnyeto amesema yupo tayari kujiunga na klabu yoyote ndani na nje ya Tanzania japo sasa hivi anaheshimu mkataba wake.
Beki huyo ambaye kwa kipindi kirefu amehusishwa kujiunga na vigogo wa soka nchini Tanzania, Simba na Yanga, hivyo kusababisha presha kwa mashabiki na wapenzi wa timu ya Coastal Union kukosa huduma yake.
Lakini kwa siku hizi za karibuni kulikuwa na taarifa kuwa beki huyo ameshajiunga na Simba SC, lakini uongozi wa Coastal Union ulikanusha taarifa hizo kuwa siyo za kweli.
Mwamnyeto alisema kwa sasa hivi akili yake ipo katika kuisaidia timu yake ya Coastal Union na anaheshimu mkataba aliokuwa nao sasa na si vingine.
Alisema yupo tayari kujiunga na timu yoyote itakayoonyesha nia ya kuhitaji huduma yake, si Simba wala Yanga pekee.
“Hakuna timu yoyote ambayo imenifuata kufanya mazungumzo na wala hakuna waliokubaliana na klabu yangu,” alisema Mwamnyeto.
Alisema kuwa malengo yake ni kucheza soka nje ya nchi ili siku moja atimize ndoto zake alizojiwekea lakini klabu itakayofikia vigezo na masharti yake basi atafanya nayo kazi.
Naye, Mwenyeketi wa Kamati ya Usajili na Mashindano wa Coastal Union, Hemed Aurora alipoulizwa juu ya suala hilo, alisema wanachofahamu hadi sasa Mwamnyeto ni mchezaji wao halali kwa sababu bado wana mkataba naye.
Aurora alisema hakuna klabu yoyote iliyoleta maombi ya kutaka kumsajili Mwamnyeto na hizo taarifa zinazosambaa hajui wanaozitoa wanazipata wapi.
Post a Comment