NA SALEH ALLY
TUKO katika wakati mgumu na tunapaswa kukubaliana na hilo hata kama tunaendelea kuchukua tahadhari kuendelea kupambana na maambukizi ya Covid 19 maarufu kama Corona.
Hapa ninazungumzia jamii ya Watanzania, jirani zetu, Afrika na dunia kote, hakika ugonjwa huu ni hatari ten asana.
Hatuna haja ya kuendelea kuficha sana na kama tuna hofu, basi ilenge katika kuchukua tahadhari huku tukihakikisha yanayowezekana yanaendelea kufanyika.
Nitalenga katika michezo ambayo pamoja na kuwa na nguvu sana, kwa sasa inaonekana kupoteza nguvu kabisa dhidi ya Covid 19 ambayo inaendelea kuyatetemesha hata mataifa makubwa ambayo yamekuwa yakitegemewa wakati wa shida.
Kusikia Marekani leo inapewa msaada, au Uingereza kulazimika kupokea misaada ni jambo la kawaida kabisa, kitu ambacho hapo awali ilikuwa si lahisi kukiona kinatokea.
Wanamichezo kwa ujumla maisha yao yamebadilika kwa asilimia kubwa kama ambavyo tunaona wanajamii wengine.
Kwa sasa fasheni au ulazima ni kufanyia kazi nyumbani. Hii yote ni kukwepa maambukizi yasiendelee kusambaa kwa kuwa yenyewe hayana nguvu ya kujisambaza isipokuwa ni watu.
Utaratibu huu ni mpya ambao haujazoeleka na mtu yoyote kabla ya hapo, ndio maana nikasema utaratibu wa maisha ya kawaida umebadilika kabisa. Wakati unaingia katika mfumo huo, kwa wengine kunaweza kuwa na mwendo tofauti lakini kwa wanamichezo, maisha lazima yawe tofauti.
Utofauti wenyewe unatakiwa kuendeshwa na nidhamu ya kiwango cha juu sana kutokana na asili ya miili ya wanamichezo. Kawaida miili yao imezoea shuluma, inataka mateso ili kuwa imara.
Muda wote wako mazoezini, baada yah apo ni mechi halafu wanarejea tena mazoezini. Ni maisha ya kuitesa miili ambayo imezoea lakini kwa sasa ni vigumu kupata nafasi kama ya awali.
Utaona baadhi ya nchi kama England, Ujerumani na chache nyingine wameanza kurejea katika mazoezi ambayo yana tahadhari kubwa nab ado hayatoi nafasi ya kufanya mazoezi kwa kiwango kile cha zamani kilichozoeleka.
Hivyo nidhamu inatakiwa kuwa juu sana la sivyo, baadhi ya nyota wanaweza kurejea wakiwa wameporomoka viwango kufikia hata kuwashangaza wapenda soka au michezo kwa ujumla.
Ambaye hana nidhamu katika chakula, nidhamu ya kuendelea kufanya mazoezi kujiweka fiti, ataonekana pale ligi zitakapozan na kukaa sawa atalazimika kutumia nguvu nyingi sana hapo baadaye.
Kwa wanasoka au wanamichezo, kwa sasa hawapati mamzozi au shuluba ya miili yao, hivyo lazima wapunguze chakula, waangalie ulaji wao kwa maana ya vyakula na ikiwezekana kupata ushauri wa madaktari nah ii ninalenga zaidi katika Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza na ligi nyingine za soka lakini wanamichezo wengine.
Nidhamu hiyo itawafanya kubaki na miili ambayo haitahitaji nguvu nyingi sana pale watakapokuwa wakirejea katika hali ya kawaida, siku ambayo tunaamini Corona itakuwa imepatiwa ufumbuzi.
Haya yote yanaweza kufanyika kwa mtu mwenye nidhamu ya kazi yake, anayejitambua na mwenye hamu ya kuendelea au kutaka kufanya vizuri katika kazi yake.
Utekelezaji wa haya ni maumivu, kwa kuwa yatamyima mchezaji ile hali ya kufanya anavyotaka na lazima kujikumbusha hili janga la Corona si likizo. Ni kipindi cha kazi ambacho tumelazimika kubadili aina ya maisha.
Kwa madaktari wa michezo au wa timu, wao wakati huu wanaweza kuwa na kazi kubwa zaidi kwa kuwa ni kipindi ambacho afya inatakiwa kupangiliwa sana. Hivyo waifanye kazi yao kwa upana zaidi na ikiwezekana kuwafuatilia wachezaji kwa ukaribu zaidi ili kuwaokoa pale watakapokuwa wanarejea wawe katika hali nzuri ambayo haihitaji nguvu nyingi kurudi katika mwendo sahihi.
Post a Comment