KAMA lengo ni kushinda mataji na kupata mshahara kwa wakati, Simba ni sehemu sahihi sana kwa Papy Tshishimbi. Tangu tajiri, Mohammed Dewji aliporejea ndani ya timu hiyo, suala la madai ya wachezaji halipo tena ndani ya Msimbazi.
Hakuna mchezaji anayedai posho wala mshahara wake, wote wanalipwa kwa wakati. Hakuna kiongozi yeyote anayedai, wote wanalipwa chao mapema tu.
Tangu Mohammed Dewji amerejea Simba, timu yenye ushindani imetengenezwa na mataji sasa imekuwa ndiyo utamaduni wa mnyama kwa misimu miwili mfululizo.
Kama Papy Tshishimbi anataka pesa kwa wakati na kuwa sehemu ya timu iliyoshinda mataji hata kama ukiwa benchi, Simba ni chaguo sahihi.
Kwa sasa ni rahisi kushinda mataji hata kama ukiwa benchi kuliko kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha Yanga. Moja kati ya kazi ngumu ambazo anaweza kukutana nazo Tshishimbi ni kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha Simba.
Hili suala gumu mno. Papy ni moja ya viungo wazuri sana lakini Simba ina wachezaji wa nafasi yake wengi na wazuri zaidi yake. Ndiyo, wako wengi na wazuri zaidi yake. Anaweza kucheza lakini atatakiwa kupambana sana.
Misimu miwili iliyopita Simba wametengeneza kikosi cha ushindani hasa. Karibu kwenye kila nafasi kuna wachezaji wawili wanaokabiliana kwa ubora.
Idara ya kiungo anakocheza Papy ndiyo hakufai. Kila mtu fundi. Ndiyo, anaweza akacheza lakini itamuhitaji ajitoe sana na bahati mbaya pia umri wake unakwenda. Yuko juu ya miaka 30, bidii sana inahitajika.
Unapoona watu wenye kiwango kama Sharaf Shiboub anakalia mkeka, fundi kama Hassan Dilunga anasugua Mbao haiwezekani Tshishimbi akapata urahisi wa kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha Simba.
Simba kwa sasa inahitaji mchezaji mwenye kitu cha zaidi ya Clatous Chama na Jonas Mkude ambacho sikioni kwa Papy. Sidhani Kama zinaweza kuwa mbinu nzuri za kuimarisha timu kwa kumleta Tshishimbi labda kama inatumika kuwakomoa Yanga.
Sina tatizo na ubora wa Tshishimbi, ni mchezaji mzuri na ana msaada mkubwa pale Yanga lakini sidhani kama atatoboa kwenye kikosi cha kwanza. Kwa aina ya wachezaji waliopo pale Simba wa idara ya kiungo, sidhani kama atawaletea kitu cha tofauti.
Kama malengo ya Tshishimbi ni kupata pesa na kulipwa mshahara wake kwa wakati, Simba ni sehemu sahihi sana kwake na hasa kwa kipindi hiki, lakini kama lengo ni kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza, basi pale sio.
Simba ina watu wengi na bora kwenye eneo hilo. Kama kupata muda kidogo wa kucheza sio tabu kwake, Msimbazi itamfaa sana.
Haruna Niyonzima alikuwa mchezaji hodari na tegemeo sana ndani ya Yanga, lakini alipokwenda Simba kwenye zama hizi alishindwa kupata nafasi. Baada ya kurudi Yanga, amekuwa tegemeo tena. Yanga bado ushindani ni mdogo sana.
Sio kwamba Haruna hakuwa bora ndani ya Simba, hapana lakini haikuwa rahisi kwake kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza. Ibrahim Ajibu alikuwa mchezaji bora na tegemeo kwa Yanga kwa misimu yote miwili akiwa huko, lakini aliporejea Simba, amekuwa mtu kula mkeka tu.
Pia sio kwamba Ajibu ni mchezaji mbaya au ameshuka kiwango, hapana. Ajibu bado ni yule yule isipokuwa kwa sasa kuna kina Ajibu wengi sana pale Msimbazi.
Sina tatizo kabisa na uwezo wa Tshishimbi, ni mchezaji mzuri lakini nadhani Simba kuna wachezaji wengi sana wa ubora wake na zaidi. Kama Tshishimbi anatafuta pesa ya uhakika, pale Simba ipo. Sina wasiwasi na uwezo wake, nina wasiwasi na yeye kupata nafasi ya kwanza kwenye kikosi.
Kupanga ni kuchagua, kuna muda mchezaji wa soka anahitaji pesa na kuna muda anahitaji kucheza. Kuna muda mchezaji anahitaji kushinda mataji, kazi kwa Tshishimbi tu. Pale kumekuwa na changamoto nyingi sana nje na ndani ya uwanja.
Sio rahisi kupata pesa na mataji kwa msimu huu lakini unaweza kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza. Yanga bado inapambana kuimarisha kikosi chake. Kama watajipanga vizuri kiuchumi na kiufundi wanaweza kushindana haswa kuanzia msimu ujao.
Misimu mitatu mfululizo, unaonekana imekuwa na ufalme wa Simba. Simba wana timu bora, hawana tatizo la kuhudumia timu. Tshishimbi anapaswa kuchanga vema karata yake.
Ni muda wa kujipanga haswa. Bado anaweza kucheza Yanga kwa misimu mingine hata mitatu, lakini akienda Simba na kuchemsha haiwezi kuwa rahisi kwake kurudi Yanga kama ilivyokuwa kwa Niyonzima.
Kuna tofauti kati ya ufalme wa Niyonimza na ufalme wa Tshishimbi pale Jangwani. Bado Tshishimbi hajazikonga hasa nyoyo za wapenzi wa Yanga.
Amekuwa na timu kwa misimu miwili na nusu sasa na hajashinda ubingwa wowote. Bado hajaacha alama pale Jangwani. Jina lake ni rahisi sana kufutika kuliko la Niyonzima.
Huu ndiyo wakati wake wa kuamua. Huu ndiyo muda wake wa kuchanga karata zake vema.
Post a Comment