HABARI kubwa kwa sasa ni suala la mchezaji wa Simba, Clatous Chama kuwindwa na watani wa jadi wa muda wote ndani ya ardhi ya Bongo ambao ni Yanga.
Mambo yamekuwa mengi ila muda unazidi kukatika taratibu kutokana na habari kuwa nyingi katika hili ila lazima ukweli uwekwe bayana na kila kitu kiwe wazi katika hili.
Mtazame ambaye ananukuliwa kwamba ndiye amesema kuwa amefanya mazungumzo na mchezaji Chama ambaye ni kiongozi mkubwa ndani ya Yanga.
Fredrick Mwakalebela yeye ni Makamu Mwenyekiti wa Yanga ni kiongozi makini ambaye anajua weledi wa kazi za masuala ya mpira pamoja na ishu zote za usajili.
Nafasi ya kuwa kiongozi ndani ya Shirikisho la Soka kwa muda mrefu inambeba na kumfanya awe na uzoefu katika masuala ya usajili achilia mbali kanuni na utaratibu wa kuzungumza.
Ni ngumu kuamini kwamba hajui anachokifanya ila ameweka wazi nia yake ilikuwa ni utani na ameomba msamaha kwa kuwa Uongozi wa Simba ulianza kuchukua hatua kwa uzito.
Kikubwa ambacho kinapaswa kiwekwe wazi hapa ni namna ya uwazi kwa wachezaji na mkataba wao unavyokuwa ili kuepusha hizi sarakasi.
Timu kubwa zimekuwa na kawaida ya kuficha mambo ila pale inapotokea tatizo ndipo kila mmoja anapotaka kutafuta pa kutokea ili amkomoe mmoja ama kuonesha kwamba yeye ni mwamba katika jambo fulani analofanya.
Wakati ule wa Papy Tshishimbi tumeona kwamba uongozi wa Yanga ulitumia busara kwa kukaa mezani na mchezaji na kuzungumza naye ila kwa sasa upande wa pili ishu ya Chama imekuwa kubwa na imegonga hodi ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Haina maana kwamba nawakataza Simba kufanya hivi hapana ila ukweli wa mkataba wa Chama upoje, ni mwaka mmoja kweli ama miezi sita imebaki hivyo kutokana na presha basi viongozi mnataka kuonyesha kwamba mpo makini katika hili kumbe ni danganya toto?
Twende katika hili tujikumbushe wakati ule kabla ya baadhi ya wachezaji kuondoka ndani ya Simba ikiwa ni pamoja na Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima twende na James Kotei hawa nyota wakati ule ilikuwa ukiwauliza wao walikuwa wanasema bado wana mkataba ndani ya Simba.
Mwisho wa siku kila mmoja alisepa zake na waliondoka bure kabisa kwa kuwa hawakuwa na mikataba ndani ya Simba na sasa wapo sehemu nyingine maisha yanaendelea hivyo katika hili la Chama linafikirisha na ni somo kuhusu uwazi wetu.
Pia tayari Mwakalebela ameomba msamaha kwa ajili ya suala hili nalo lisipuuzwe kwa kuwa aliamini ni utani, kwa sasa ni lazima iwe fundisho kwa wengine na kutazama mipaka ya utani.
Post a Comment